Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imewaaga wahitimu 26 wa mafunzo tarajali wa kampuni hiyo kwa mwaka 2021/2022 ambazo hutekelezwa kila mwaka kwa kushirikiana na ofisi ya Waziri Mkuu (ajira, vijana, na watu wenye ulemavu), Mfuko wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na Chama cha Waajiri Nchini (ATE).
Akizungumza mkoani Geita, katika hafla ya kuwaaga wahitimu hao Meneja Mwandamizi anayesimamia kitengo cha Afya, Usalama, Mazingira na Mafunzo wa GGML, Dkt. Kiva Mvungi amewapongeza wahitimu hao kwa kufikia hatua hiyo muhimu kwa fani walizozisomea.
Amesema, “Tunawapongeza kwa kupata fursa hii. Kwa ambao mlichangamkia fursa za ajira zilipotangazwa, tunawapongeza kwa kuwa wafanyakazi wa kudumu wa kampuni hii. Kwa ambao bado hamjapata ajira, endeleeni kutuma maombi yenu kila GGML inapotoa nafasi za kazi,”
Aidha, Dkt Mvungi ameongeza kuwa, “Kukamilisha programu hii ni mwanzo sasa wa kuonesha ukomavu wenu mnapoitwa katika udahili wa kazi. Asimilia kubwa ya vijana waliopitia programu hii wameajiriwa na makampuni mbalimbali, bila shaka nanyi mtaajiriwa pia hapa GGM au kwingineko. Lengo letu ni kuhakikisha kuwa sekta ya madini hapa nchini inapata wafanyakazi wenye uzoefu.”
Naye, Mhandisi Ruth Mugurusi, wa kitengo cha ulipuaji GGML amesema, “Ninaishukuru sana GGML kwa kunipatia fursa hii. Baada tu ya kuhitimu masomo yangu ya Chuo Kikuu, nilituma maombi na kuanza mafunzo haya. Namshukuru Mungu nikiwa katika kipindi cha mafunzo haya, zilitangazwa nafasi na mimi na wenzangu tukatuma maombi na kufaulu usaili na leo hii hatimaye tumeajiriwa na GGML.
Tangu programu hii ianze mwaka 2009 hadi hivi sasa jumla ya wahitimu 168 wamenufaika ambapo kati ya hao wasichana ni 58 na wavulani ni 110. Asilimia kubwa wameajiriwa na GGML katika vitengo vya uchenjuaji dhahabu, uhandisi, ufundi, ulipuaji na uchimbaji madini na baadhi yao wameajiriwa katika makampuni mengine ndani na nje ya nchi.