Mshabuliaji wa Arsenal Olivier Giroud amewapa mashabiki wa timu hiyo kile ambacho huenda wakakosa kutoka kwake baada ya kuifungia bao katika ushindi wa 3-1 dhidi ya timu ya Western Sydney Wanderers.
Arsenal wapo nchini Australia ambapo wameweka kambi ya maandalizi ya msimu ujao na huu ni mchezo wao wa pili wa kirafiki nchini humo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Sydney katika mchezo wa kwanza.
Olivier Giroud anahusishwa na kutaka kuondoka Arsenal kuelekea Borussia Dortmund hasa ikizingatiwa kuwa Arsenal tayari wamemsajili Alexandre Lacazette kutoka Lyon.
Giroud aliipatia Arsenal bao la kuongoza dakika ya 33 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Monreal kabla ya Aaron Ramsey kuogeza bao la pili katika dakika ya 37.
Kabla ya kipindi cha kwanza kuisha mchezaji kutoka Misri Mohamed Elneny aliipatia Arsenal bao la tatu dakika ya 44 baada ya kupiga shuti kali lililomgonga mchezaji wa West Sydney Wanderers na kutinga wavuni.
Bao pekee la timu ya West Sydney Wanderers limefungwa na mchezaji Lusticas katika dakika ya 57 na kufanya mchezo huo kumalizika kwa Arsenal kushinda 3-1