Kuelekea mchezo wao wa mkondo wa pili wa Hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Kaizer Chifes utakaochezwa kesho Jumamosi (Mei22), Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes, amesema ana matarajio makubwa kutoka katika kikosi chake na kwenye mchezo wa soka hakuna kisichowezekana.
Gomes ameeleza kuwa alifanya makosa katika mchezo wa kwanza kwa kutumia viungo wawili ambao walikuwa wakiziba nafasi na kuwafanya wapinzani wao kucheza mipira ya juu.
Kocha huyo amesema tayari amefanyia kazi mapungufu ya kikosi chake na anatarajia watafanya vizuri katika mechi ya kesho endapo wachezaji wake watajitoa kwa kiwango kikubwa katika mchezo huo ambao wanahitaji ‘kupindua meza kibabe’.
“Wao wametufunga kwao mabao 4-0, nakiri hatukucheza vizuri hasa kwenye safu ya ulinzi kitu ambacho benchi la ufundi limefanyia kazi kuondoa makosa yote, tunapaswa kupambana kiume, wachezaji, benchi la ufundi, viongozi pamoja na mashabiki tunatakiwa kujua kwenye mpira kila kitu kinawezekana na tunajiandaa kufanya vizuri,” amesema Gomes.
Ameongeza wamejiandaa kuingia dimbani tofauti na walivyocheza ugenini na amewataka mashabiki kuondoa hofu.