Kocha mkuu wa klabu ya Simba SC Didier Gomes Da Rossa amesema mlinda mlango Aishi Manula ataendelea kuwa sehemu ya kikosi chake, licha ya kuhusishwa na taarifa za kuwaniwa na klabu ya Al Merrikh ya Sudan.
Manula amekua akitajwa kumvutia kocha mpya wa Al Merrikh Lee Clark, ambapo inadaiwa tayari ameshaushinikiza uongozi wa klabu hiyo kufanikisha mpango wa kumsajili kwa msimu ujao wa Ligi ya Sudan na michuano ya kimataifa endapo watafuzu.
Taarifa zinasema kuwa uongozi wa klabu hiyo umetenga dola za kimarekani 100,000 sawa na milioni 230 kwa pesa za Tanzania, kama ada ya usajili wa mlinda mlango huyo, ambaye pia ni chaguo la kwanza la timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.
Kocha Gomes ambaye alijiunga na Simba SC mwezi Januari 2021 akitokea Al Merrikh amesema haamini kama kuna ukweli kwenye taarifa hizo, kwa sababu anaifahamu vyema klabu hiyo ambayo aliitumikia kuanzia mwaka 2020-2021.
“Ninaifahamu vizuri Al Amerrikh, nimefanya kazi pale kwa muda mrefu, sina uhakika kama taarifa hizo zina ukweli wowote, kwa sababu kuna watu wengi wanakua na tabia ya kuzusha mambo.”
“Nikuhakikishie Manula ataendelea kuwa sehemu ya kikosi cha Simba kwa miaka mingi zaidi, ninaamini hilo kwa sababu ni mchezaji muhimu na anaipenda sana Simba.” Amesema Kocha Gomez.
Manula mpaka sasa amefungwa bao moja kwenye michezo minne aliocheza ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya makundi, huku mchezo mmoja dhidi ya Al Merrikh uliochezwa Khartoum, Sudan akicheza Beno Kakolanya.