Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, Didier Gomes da Rosa, bado anaweweseka na kichapo cha bao 1-0 alichokipokea kutoka kwa Young Africans siku ya Jumamosi (Julai 03).
Kocha Gomes ambaye kabla ya mchezo huo uliounguruma kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, alikua na rekodi ya kukiongoza kikosi chake pasina kufungwa mchezo wa Ligi Kuu tangu alipoajiriwa Simba SC mwanzoni mwa mwaka huu, amesema hakutarajia kama angepoteza mbele ya Young Africans.
Kocha huyo kutoka nchini Ufaransa amesema kitendo cha kuangusha alama tatu dhidi ya Young Africans kimemuumiza na yupo tayari kuwajibika kwa namna yoyote.
“Nipo tayari kuwajibika katika hili kwa nafasi yangu ya ukocha, kwani si jambo zuri kupoteza mechi kubwa ya namna hii ambayo ndani yake ilikuwa na rekodi nyingi bora kama tungepata ushindi.”
“Kipindi cha kwanza tulicheza kwa kiwango cha chini jambo ambalo hata upande wangu ilinishangaza licha ya kutenga muda mwingi kuiangalia Young Africans namna walivyocheza mechi zao za mwanzo.
“Jambo jingine tulipata nafasi za kufunga wachezaji wangu walishindwa kuzitumia vizuri na kuwafanya wachezaji wa timu pinzani kuendelea kujiamini.”
Hata hivyo kocha Gomes amesema hana budi kuelekeza nguvu katika michezo ya Ligi Kuu iliosalia, ili kufikia lengo ya kuwapoza machungu mashabiki na wanachama wa Simba SC kwa kutwaa ubingwa wanne mfululizo.
“Tutaweka nguvu kwa ajili ya mechi ya KMC, ili kupata ushindi pamoja na michezo mingine mitatu iliyo mbele yetu dhidi ya Coastal Union, Azam na Namungo ili kuchukua ubingwa kama malengo yetu yalivyo.”
Ushindi wa juzi Jumamosi (Julai 03) umeiwezesha Young Africans kufikisha alama 70, huku ikisaliwa na michezo miwili mkononi kabla ya kumaliza msimu huu 2020/21 baadae mwezi huu.
Simba SC yenye alama 73 inaendelea kubaki kileleni mwa msimamo, huku ikibakiza michezo minne mkononi kabla ya kumaliza msimu huu 2020/21 baadae mwezi huu.