Kiungo kutoka nchini Brazil na Klabu ya Singida Big Stars Bruno Gomez Baroso, amekanusha taarifa za kuwa mbioni kusajiliwa na Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, mwishoni mwa msimu huu 2022/23.
Tetesi za Kiungo huyo kuhusishwa na Young Africans ziliibuka juzi Jumatano (Machi 15), baada ya kuchapishwa kwenye Gazeti la Mwanaspoti, huku ikidaiwa tayari viongozi wa pande zote wameshakubaliana sehemu ya biashara ya usajili wa Gomez.
Hiyo ni mara ya pili kwa Young Africans kuhusishwa na Mbrazil huyo, ambaye amefunga mabao tisa hadi sasa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, awali walihusishwa wakati wa Usajili wa Dirisha Dogo.
Akizungumza na Dar24 Media, Gomes amesema anachotamani hivi sasa ni kuona anaiwezesha Singida Big Stars kumaliza ikiwa katika nafasi za juu katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Gomes amesema hadi hivi sasa hakuna klabu yoyote ya Tanzania iliyomfuata kwa ajili ya mazungumzo, licha ya tetesi nyingi kuzagaa yeye kumalizana na Young Africans.
“Hakuna timu yoyote inayocheza Ligi hapa Tanzania iliyonifuata kutaka huduma yangu, licha ya tetesi kuwepo kuwa Young Africans imenifuata na kuipa ofa ya kuichezea kwa misimu miwili.”
“Hivi sasa ninachotamani ni kufanya kazi kwa bidii na kuisaidia Singida Big Stars kuwa katika nafasi ya juu kwenye msimamo wa Ligi na kulikuza jina la Singida Big Stars.”
“Ninataka kuona jina la timu linakuwa kwa mimi nikiwepo hapa nikindelea kuvalia jezi ya Singida Big Stars, huku nikikumbukwa kwa kile nilichokifanya hapa,” amesema Bruno
Kiungo huyo amekuwa akifunga mabao makali kwa njia ya faulo akimfunga kipa wa Simba SC Aishi Manula na yule wa Azam FC, Iddrisu Abdulai.