Meneja wa Klabu Bingwa Barani Ulaya Manchester City Pep Guardiola hatarajii kusaini mkataba mpya wa kuifundisha Klabu hiyo baada ya mkataba wake wa sasa na klabu hiyo utakapofikia ukomo mwaka 2025.
Kwa mujibu wa chanzo kilicho karibu na Meneja huyo kutoka nchini Hispania kinasema kuwa, bado hajafanya maamuzi juu ya hatima yake lakini anaelekea kuhitimisha muda wake kwenye klabu hiyo baada ya misimu miwili zaidi.
Anatazamiwa kuchukua jukumu la kufundisha timu ya taifa baada ya kuwindwa na Brazil na Marekani.
Guardiola alisaini mkataba mpya na Manchester City mwezi Novemba, baada ya kusafiri kwenda Abu Dhabi wakati wa mapumziko kupisha fainali za Kombe la Dunia.
Meneja huyo wa zamani wa Klabu za Barcelona na Bayern Munich amepuuza taarifa kwamba anaweza kuachana na klabu hiyo wakati huu wa majira ya kiangazi akiwa ameshinda mataji matatu, akiwahakikishia mashabiki wa City kuwa ataendelea kuinoa timu hiyo msimu ujao.
Lakini vyanzo vyanzo viliiambia ESPN kwamba kocha huyo tayari amekaa kwenye klabu hiyo muda mrefu kuliko alivyotarajia wakati akipewa kazi Februari mwaka 2016 na ana shaka kama ataweza kufanya majadiliano ya kusaini mkataba mpya majira yajayo ya kiangazi Msimu ujao utakuwa wa nane kwake ndani ya City.
Alitumia miaka minne kwenye klabu ya Barcelona na miaka mitatu kwenye klabu ya Bayern Munich.