Tume huru ya kitaifa ya uchaguzi nchini Guinea (CENI), imeanza kutangaza matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika siku ya Jumapili, Oktoba 18.
Takwimu hizo zilizotangazwa zinahusu baadhi ya maeneo tu ya majimbo 38 ya nchi hiyo ambapo katika majimbo manne, rais anayemaliza muda wake Alpha Condé ndiye anayeongoza.
Kulingana na matokeo yaliyochapishwa na Tume ya Uchaguzi Conde anaongoza katika majimbo ya Matoto, Matam, Kaloum, katika mkoa wa Conakry na Boffa, katika mkoa wa Boke.
Chama kikuu cha upinzani cha UFDG, ambacho kinadai kimeshinda kulingana na takwimu zake, kilifanya mkutano na waandishi wa habari kuelezea utaratibu watakaotumia.
Wakati huo huo, waangalizi wa kimataifa kutoka Umoja wa Afrika na ujumbe wa jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS), wamesema kuwa uchaguzi wa urais uliofanyika nchini Guinea Conakry Jumapili iliyopita ulikuwa huru na haki.
Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Conakry, Mkuu wa Ujumbe wa ECOWAS, Waziri Mkuu wa zamani wa Cape Verde José Maria Neves amesema kuwa licha ya kasoro mbalimbali zilizojitokeza, uchaguzi huo ulifanyika katika hali tulivu, huku akiwataka wanasiasa kusubiri matokeo kupitia tume ya Uchaguzi, CENI.
Haya yanajiri wakati hali ya wasiwasi ilishuhudiwa jana katika mji wa Conakry baada ya polisi kuvamia eneo la makazi ya kiongozi wa upinzani Cellou Dallein Diallo, aliyejitangaza mshindi wa uchaguzi huo.