Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini zimehimizwa kuendelea kutoa fursa sawa kwa Wanawake na wanaume kushiriki nafasi za uongozi na maamuzi katika ngazi ya jamii na kuwa sehemu ya maamuzi kwa ustawi wa jamii na Taifa.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima wakati akizindua Baraza la Taifa la Uwezeshaji wanawake kiuchumi huku akiahidi ushirikiano wa Serikali kwa Baraza hilo katika kumkwamua mwanamke kiuchumi.
Amesema, Viongozi wa Jukwaa hilo wanatakiwa kuhakikisha fursa zinazoibuliwa zinawafikia wanawake hasa waliopo vijijini na kuongeza kwamba Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi hali itakayowasaidia kushiriki kwenye nafasi za uongozi.
“Jukwaa hili lihakikishe Wanawake wote wanaona na kupata fursa ya kujiunga na majukwaa yaliopo kuanzia ngazi ya kijiji/Mtaa, Kata, Wilaya hadi Taifa, ili yawawezeshe kupata sehemu ya kujadili mambo yao kuhusu ujasiriamali na biashara kwa ujumla,” amebainisha.
Aidha, Dkt. Gwajima pia ametoa wito kwa Halmashauri za Wilaya, Manispaa na Majiji kuendelea kutenga fedha za ndani, ili kuwawezesha Wanawake,Vijana na Watu wenye ulemavu kukopa na hatimaye kuweza kujiendeleza kiuchumi.