Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma, amelitaka Bunge kutokuwa wakala wa kupitisha ‘dili’ za watu wanaoinyonya Serikali kwa kuanzisha mambo ambayo yanaliletea Taifa hasara na kwamba haoni sababu ya kufunga heleni Ng’ombe huku akipendekeza waanze na kuku ili waone mfano.
Kasheku ameyasema hayo hii leo Bungeni jijini Dodoma, wakati akichangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kuongeza kuwa ujaribishaji wa kila hatua kwa Wanyama wanaomilikiwa na Masikini haufai na badala yake waanzie kwa mifugo ya watoa wazo kwanza ili kupata matokeo yatakayokuja na muafaka.
“Wakati mwingine tutumie tu akili ya mtaani haiwezekani Ng’ombe akiibiwa Shinyanga ukajua ipo Mtwara kwa kuifunga Heleni, au Ng’ombe zikipigana kule porini hereni ikadondoka utajua imepigana na nani? hebu tuache haya jamani mmemaliza ya wamachinga sasa mnaingia kwa wafugaji, mimi sipingi agizo la Waziri Mkuu msininukuu vibaya ila tunaboresha,” amesema Musukuma.
Aidha, Musukuma pia amemtaka Waziri wa Mifugo na Uvuvi kutoingia mtego wa kukubali kupitisha mambo ambayo yanaweza kumuingiza matatani kwani wapo watu ambao wamekaa kwa ajili ya upigaji na si kulitakia mema Taifa na jamii ya masikini.