Baada ya kuanza vyema ligi kuu ya soka Tanzania bara msimu wa 2017/18 kwa kuibanjua Ruvu Shooting mabao saba kwa sifuri, mkuu wa idara ya habari na mawasilino wa klabu ya Simba Haji Sunday Manara amefichua siri ya mafanikio hayo.
Manara amesema mipango thabiti iliyowekwa na benchi lao la ufundi linaloongozwa na kocha Mcameroon Joseph Omog ni kichocheo kikubwa cha kuanza vyema ligi kuu msimu huu, kwa dhamira ya kurejesha heshima ya ubingwa huko Msimbazi.
Manara amesema kilichofanyika kwenye kikosi cha Simba ni kuundwa kwa mfumo wa safu tatu za kikosi chao kwa kipindi kirefu, huku wakithibitisha kwa vitendo maandalizi yao waliyoyafanya katika michezo ya kirafiki tangu waliporejea kutoka Afrika kusini walipokua wameweka kambi kabla ya kucheza ana mahasimu wao Young Africans katika mchezo wa Ngao ya Jamii.
“Benchi letu la ufundi limefanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha safu zote tatu zinakaa sawa, na kazi hii haikufanyika kwa siku moja kutokana na uhalisia wa mchezo wa soka, kazi hii ilianza kufanywa tangu msimu uliopita baada ya Omog kukubali kufanya kazi na Simba.
“Unajua kuunda kikosi kwa kuzingatia safu zako, naweza kuifananisha hatua hii kama uumbwaji wa binadamu, ukimtazama binaadamu unaona vitu kadhaa ambavyo viliumbwa kwa utaratibu ambao mwenyezi mungu anastahili sifa, sasa ndivyo ilivyo kwa samba SC.
“Mimi ninaimani kubwa sana kinachofanywa na kocha huyo kutoka Cameroon, nauhakika msimu huu hakuna kitakachoweza kutuzuia kufanya vizuri kwenye michuano yote tutakayoshiriki”.
“Mpaka sasa hatujaruhusu nyavu zetu kuguswa na mpinzani yoyote tuliecheza nae ndani ya dakika 90, hiyo inaashiriki kikosi chetu kimesukwa na kusukika kisawa sawa” Amesema Manara.
Tangu kikosi cha Simba kiliporejea nchini kikitokea Afrika kusini, kimeshinda michezo yote pasina kuruhusu nyavu zao kuguswa na mpira uliopigwa na wapinznai wao ndani ya dakika 90.
Simba walicheza na mabingwa wa soka kutoka Rwanda Rayon Sports na kuibuka na ushindi wa bao moja kwa sifuri, kisha wakacheza dhidi ya Mtibwa waliokubali kufungwa bao moja kwa sifuri, wakatoka sare bila kufungana na Mlandege ya Zanzibar kabla ya kuibanjua Gulioni FC mabao matano kwa sifuri.
Baada ya michezo hiyo ya kirafiki, kikosi cha Simba kilicheza dhidi ya Young Africans katika mchezo wa kuwania Ngao Ya Jamii na kuibuka na ushindi wa penati tano kwa nne, na siku kadhaa baadae kilianza ligi kwa kuichapa Ruvu Shooting mabao saba kwa sifuri.