Msemaji wa Young Africans Haji Sunday Ramadhan Manara anaamini Baadhi ya Waandishi wa Habari na Wachambuzi wa Soka la Bongo wanatumika kuwavuruga Mashabiki na Wanachama na klabu hiyo, kupitia Vyombo vya Habari na Mitandao ya Kijamii kwa maslahi ya wanaowatuma kufanya hivyo.
Manara ametoa kauli hiyo alipozungumza kupitia Yanga TV leo Jumanne (Mei 10), akiwatuliza baadhi ya Wanachama na Mashabiki wa Young Africans ambao wameonyesha kuwa na hasira kufuatia matokeo ya sare dhidi ya Tanzania Prisons jana Jumatatu (Mei 09).
Manara amesema Baadhi ya Waandishi wa Habari na Wachambuzi wa Soka la Bongo wanafanya shughuli hiyo kwa makusudi ili kuona Young Africans inapoteza muelekeo wa kutwaa ubingwa msimu huu.
“Wapinzani wetu ndicho wanachokitafuta, baadhi ya Waandishi na Wachambuzi huko mitandaoni wanawavuruga vuruga, wanawapa maneno, na nyinyi mnajaa!” amesema Manara akiwaambia Mashabiki na Wanachama wa Young Africans
“Twendeni kwenye umoja wetu, turudi mstarini, twendeni tukashinde hii mechi inayofuata. Wachezaji wamefanya kila kitu, mwingine nimeona anamlaumu Saido, anasema Saido anacheza hovyo kabisa, jamani huu mpira wa wapi huu!” ameongeza Manara
Sare ya bila kufungana dhidi ya Tanzania Prisons, imekua sare ya tatu mfululizo kwa Young Africans baada ya kubanwa na Simba SC Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumamosi (April 30), Kisha Ruvu Shooting Uwanja wa Lake Tanganyika (Mei 04).
Licha ya kuambulia matokeo ya sare bila kufungana katika michezo mitatu mfululizo, bado Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 56, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama 46.