Msemaji wa Young Africans Haji Sunday Manara amesema alikua akifanya kazi ya kuwadanganya Mashabiki na Wanachama wa Simba SC kwa kuwaambia klabu yao ni kubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa kuwa na mataji mengi kuliko klabu nyingine yoyote kwenye ukanda huo.
Manara amelisema suala hilo alipohojiwa kwenye kipindi cha Sports HQ kupitia Radio EFM, kufuatia kauli tata ambazo zimegongana wakati huu akiwa Young Africans, na wakati ule akiwa kwa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, kuhusu mataji ya michuano katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati.
Manara amesema kazi kubwa aliyokua anaifanya Simba SC ni kubuni mbinu za kudanganya na ameutaka umma wa wadau wa soka nchini kutambua alikua hafanyi jambo jema kwa kubuni uongo, ambao alikua anawaaminisha Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo ya Msimbazi.
“Moja ya kazi kubwa niliyoifanya labda ni kuonesha ukubwa feki hiyo dhambi niliitenda vibaya sana, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nipo inihukumu kwa kifungio cha gerezani kwa kufanya ulaghai wa kufix ukubwa ambao hata haupo.”
Baada ya kusema hivyo Haji akaongeza kuwa, kwa sasa amekua mkweli na ndio maana ameitaja Young Africans kama klabu inayoongoza kwa kutwaa mataji mengi Zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, vinginevyo ni uwongo ambao hapo nyuma alishiriki kuupika.
Haji Manara aliibua malumbano mitandaoni jana Jumatano (Septemba 08) baada ya kuitaja Young Africans kama klabu iliyotwaa mataji mengi katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati, huku wengine wakikumbushia aliwahi kusema maneno kama hayo alipokua Simba SC.