Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Morocco Hakim Ziyech yupo kwenye mazungumzo binafsi na Uongozi wa Mabingwa wa Soka nchini Ufaransa Paris Saint-Germain ‘PSG’.
Kwa mujibu wa Gazeti la L’Équipe la Ufaransa, Kiungo huyo anatarajiwa kuuwahi muda wa Dirisha Dogo la Usajili kabla haujamalizika leo Januari 31, ili kukamilisha uhamisho wake kutoka Chelsea.
PSG inayoongoza msimamo wa Ligi ya Ufaransa ‘Ligue 1’, imeripotiwa kufanya mazungumzo na Chelsea ya kumsajili Ziyech, na kinachoendelea kwa sasa ni muhusika kukubaliana masuala binafsi huko jijini Paris.
Usajili wa Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 29 una dhamira ya kuziba nafasi ya Pablo Sarabia aliyesajiliwa Wolverhampton Wanderers ya England, baada ya kupelekwa kwa mkopo Sporting CP ya Ureno msimu wa 2021/22.
Ziyech aliyewahi kuitumikia ajax Amsterdam kabla ya kusajiliwa Chelsea mwaka 2020, amekua na wakati mgumu wa kuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha The Blues, akicheza michezo 56 na kufunga mabao 6.