Taarifa ya uchunguzi wa sakata la mtoto kugeuka jiwe Musoma, imethibitisha kuwa hakuna mtu aliyezaa jiwe wala mtoto aliyegeuka jiwe bali mzazi Amina Abdallah aliyemuahidi kumzalia mumewe mtoto wa kiume aliamua kuokota jiwe na kulipeleka kwa wakwe na kuzusha alizaa mapacha lakini mtoto wa kiume aligeuka jiwe.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Khalfany Haule na kuongheza kuwa Amina ambaye ni Mkazi wa Katoro Chato, alihamia kijiji cha Mwabuki Bariadi na Machi 27, 2023 alijifungua Mtoto wa kike Zahanati ya Mwabuki na si mapacha.
Jiwe linalodaiwa kuwa lilikuwa ni mtoto wa kiume.
Amesema, “huyu Hamisi yupo Dar na alituma nauli ili watoto wapelekwe kwa Bibi yao Buhare Musoma, Amina alianza safari April 13,2023 akiwa na jiwe alilolichukua kwenye mawe ya ujenzi, alifika Musoma na kuzusha mtoto wake pacha aitwaye Amiri ameguka jiwe na kutaka azikwe usiku huohuo ili kuondoa mikosi.”
“Kamati imejiridhisha kuwa Amina alikuwa na makubaliano na Hamisi ya kumzalia Mtoto wa kiume tangu mwanzo wa mahusiano yao hivyo Hamisi akaendelea kulea mimba akitarajia Mtoto wa kiume, baada ya kujifungua Mtoto wa kike, Amina aliendelea kumwaminisha Hamisi kuwa amejifungua pacha wa kike na kiume kumbe si kweli.”