Rwanda imeripoti kutokuwa na visa vipya vya virusi vipya vya corona (covid-19) ikitangaza majibu ya vipimo vya sampuli 896 yaliyotolewa jana, Mei 5, 2020.
Majibu hayo yaliyotolewa na Serikali ya Rwanda yameonesha utofauti mkubwa kutokana na matokeo ya hivi karibuni yaliyokuwa yanaonesha kuongezeka kwa visa vipya vya corona.
Visa vingi vilivyokuwa vimeripotiwa vilielezwa kuwa vimetoka kwa madereva wa malori yanayotoka nchi jirani.
Hivi karibuni, Serikali ya Rwanda ilitangaza kupunguza masharti ya kubakia nyumbani. Iliruhusu baadhi ya shughuli kuendelea kwa masharti maalum yenye tahadhari.
Iliwataka wananchi wake kuendelea kuvaa barakoa, kunawa mikono mara kwa mara kwa sabuni na maji yanayotiririka na kuweka umbali kati yao.
Hadi sasa duniani kote kuna visa 3,743,654, waliopona ni 1,248,705 na vifo 258,850 vitokanavyo na virusi vipya vya corona (covid-19).