Benchi la Ufundi la Young Africans limelazimika kubadili Programu ya mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya 2021/22 ambao utaanza rasmi mwezi Septemba .
Young Africans imeweka kambi nchini Morocco na jana Jumanne (Agosti 17) ilianza maandalizi chini ya kocha Nabi.
Mkuu wa Idara ya Habari ya Young African Hassan Bumbuli, ambaye hata hivyo hakusafiri na timu, amesema amepokea taarifa kutoka kwa kocha mkuu kwamba hali ya joto kali katika mji huo imesababisha kubadili programu yao ya mazoezi.
“Kocha amesema wamefanya mazoezi asubuhi kwa muda mchache kutokana na joto kali, hivyo kuanzia leo, watalazimika kufanya mazoezi mapema sana asubuhi kabla ya jua kuchomoza na kisha hali ikiruhusu baada ya jua kuzama jioni.
Hali ya jijini Casablanca ilipo kambi ya Young Africans kwa sasa inaelezwa ni joto kali tofauti na kambi ya Simba ilipo jijini Rabat nchini humo, ambayo haitofautiani sana na Dar es Salaam kwa sasa.
Kuhusu wachezaji ambao walikuwa hawajajiunga na kikosi hicho, Bumbuli amesema ni wachezaji wawili tu, ambao ni Khalid Aucho na Yannick Bangala Litombo, ambao wanatarajiwa kuwasili Morocco leo Jumatano (Agosti 18).
Young Africans inajiandaa na Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja ba Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, ambapo wamepangiwa kuanza na Rivers Unites ya Nigeria mwezi Septemba.