Baada ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kumkemea kanisani mbunge wa Kawe, Halima Mdee kuhusu tuhuma za kumtolea lugha chafu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mbunge huyo amejibu.
Katika ibada ya Jumapili, Gwajima alimtaka Mdee kumuomba radhi spika, Job Ndugai na kueleza kuwa kitendo alichokifanya cha kutoa lugha chafu dhidi ya kiongozi huyo wa mhimili sio sahihi.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Mdee amekanusha tuhuma hizo na kueleza kuwa hajamtukana Spika wa Ndugai na kwamba hatarajii kufanya hivyo.
“Namuheshimu sana Mch.Gwajima, sitajibizana nae kwenye mitandao. Niweke rekodi sawa sijamtukana na wala sitarajii kumkosea heshima Spika,” aliandika Mdee.
“Hayo ya J2 namwachia yeye! Yangu na yaliyojiri Bungeni.. Najua jinsi ya kuyahandle. Yawezekana yalishamalizwa kabla ya Ibada yake LEO,” aliongeza kwenye tweet nyingine.
Kutokana na tuhuma za kutoa lugha chafu, Spika Ndugai aliamuru Mdee akamatwe popote alipo au ajisalimishe bungeni mapema kujibu tuhuma hizo. Mdee alifika bungeni mjini Dodoma na kujieleza mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu tuhuma hizo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe pia alihojiwa na Kamati hiyo kwa tuhuma za kutoa maneno yasiofaa dhidi ya Spika wa Bunge na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.