Shirikisho la soka nchini TFF bado halijapokea taarifa rasmi kuhusu ushiriki wa timu ya taifa ya Mali kwenye fainali za vijana chini ya umri wa miaka 17 zitakazofanyika nchini Gabon Mei 14-28 mwaka huu.

Mali imefungiwa na FIFA kwa muda usiliojulikana, baada ya serikali ya nchi hiyo kuingilia mchezo wa soka, kwa kuweka kamati ya muda ya uongozi wa shirikisho la soka nchini humo, na kutangaza kutowatambua viongozi walioingia madarakani kwa mujibu wa katiba.

Mkurugenzi wa ufundi wa shirikisho la soka nchini TFF Salum Madadi, amezungumza na Dar24 kuhusu sintofahamu hiyo, ambapo amesema mpaka sasa hawajafahamu kama Mali watashiriki ama hawatashiriki.

“Hatupendi kusikia kuhusu kuondolewa kwa Mali katika michuano hii, kwa sababu tunataka kundi na Serengeti Boys kuwa na timu nne ili tuwe na nafasi ya kucheza kwa kupambana kwenye michezo mitatu ya hatua ya makundi.

“Ni kweli tumesikia wamefungiwa na FIFA, lakini CAF ambao ni wasimamizi wa michuano ya AFCON kwa vijana, hawajatuandikia barua ama kutuletea taarifa zozote kuhusu mustakabali wa Mali kushiriki michuano hii. Tunaendelea kusubiri” Amesema Madadi.

Serengeti Boys wamepangwa katika kundi B lenye timu za Niger, Angola na Mali. Endapo Mali wataondolewa kwenye michuano hiyo kundi hili litabaki na timu tatu hali ambayo itaifanya kila timu shiriki kucheza michezo miwili badala ya mitatu.

Serengeti Boys imeweka kambi mjini Rabat-Morocco tangu juma lililopita na itakua huko mwa mwezi mmoja kabla ya kuelekea nchini Cameroon kwa siku kadhaa, na kisha itasafiri hadi nchini Gabon tayari kwa michuano ya vijana ya Afrika.

CUF hali si Shwari, Maalim atoa tamko zito
Halima Mdee amjibu Gwajima