Imeelezwa kuwa Kilimo cha Umwagiliaji ni chanzo kikubwa cha mapato katika Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara kwani huingiza shilingi Milioni mia moja ishirini (120) hadi milioni miambili (200) kwa mwaka na kuinua pato la wananchi wilayani humo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Yefred Myenzi ambapo amesema kuwa serikali ilitoa kiasi cha takribani shilingi Bilioni 2.2 kwa ajili ya ujenzi na maboresho ya Skimu za Umwagiliaji sambamba na kuwawezesha wakulima kupata elimu ya kilimo, uendeshaji na matunzo ya miundombinu ya umwagiliaji, jambo ambalo limepelekea wananchi kujikita zaidi kwenye kilimo cha umwagiliaji na kuongeza pato la halmashauri.
“Mazao mengi yanayolimwa katika Skimu za umwagiliaji ni mpunga na mazao menginge ya Mboga mboga, lakini pia kuna mazao ambayo hayalimwi katika Skimu hizo kama vile Mtama, Uwele na Shayiri zao ambalo linatumika kama malighafi katika viwanda vingi vya bia hapa nchini.”amesema Myenzi
Amesema kuwa Skimu hizo zimesaidia kuwepo na chakula cha kutosha na Usalama wa chakula katika Wilaya hiyo, pamoja na kwamba Kilimo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na Skimu hizo kuwa mbali na masoko, jambo ambalo linapelekea kupanda kwa gharama za usafirishaji wa mazao kwenda kwenye masoko na kukosekana kwa bei ya uhakika.
Kwa upande wake, Mhandisi wa Kanda ya Dodoma ya Umwagiliaji inayohusisha mikoa ya Dodoma, Singida na Simanjiro, Lucy Lema amesema kuwa Serikali ina mikakati kabambe ya kuendeleza kilimo hicho kwa kufanya upanuzi wa maeneo na kufanya tafiti kabla ya ujenzi wa mabwawa, kufanyia ukarabati wa Miundombinu ya Umwagiliaji na kuendeleza Skimu ndogo ndogo za umwagiliaji kupitia miradi mbalimbali.