Halmashauri nchini, zimekusanya Jumla ya Shilingi Bilioni 485.42 ambazo ni sawa na asilimia 48 ya lengo la mwaka na asilimia 96 ya lengo la nusu mwaka, kwa kipindi cha mwezi July – December 2022 kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Hayo, yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angellah Kairuki jijini Dodoma, wakati akiwasilisha taarifa ya ukusanyaji wa Mapato ya ndani katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2022/23 kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti.
Amesema, katika makusanyo hayo mapato yasiyolindwa ni shilingi Bilioni 396.67 na mapato lindwa ni shilingi bilioni 88.73 ambapo katika mwaka wa fedha wa 2022/23, Halmashauri ziliidhinishiwa kukusanya shilingi Trilioni 1.02 kutoka kwenye vyanzo vya ndani.
Aidha, Kairuki pia ameongeza kuwa, makisio ya mapato ya ndani yaliongezeka kutoka Shilingi Bilioni 863.90 mwaka 2021/22 hadi Shilingi Trilioni 1.012 mwaka 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 17 likiwa ni ongezeko la Shilingi Bilioni 148.