Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo ametoa wito kwa wakurugenzi wote nchini kutoa kipaumbele kwa sekta ya mazingira kwa kutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa miche ya miti.
Dkt. Jafo ametoa wito huo alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua Mradi wa ujenzi wa josho la kuogeshea mifugo katika Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma hii leo Aprili 13, 2023 na kuongeza kuwa kumekuwa na changamoto kwa maafisa mazingira Wilaya kutokuwa na bajeti ya kwa ajili ya shughuli za upandaji miti.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo (katikati).
Amesema, maafisa hao wilayani kuwa wana kazi kubwa ya kuhakikisha maeneo yao yanapandwa miti ili kukabailiana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kwamba kipaumbele cha afisa mazingira ni mazingira yenyewe hivyo ni wakati sasa wa kila halmashauri kuwa na bajeti kwa maafisa hao ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao.
“Serikali inapambana kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa, hivyo na afisa mazingira anatakiwa awe na nguvu hata siku ikitokea apande miti elfu tatu basi awe na bajeti. tunatarajia afisa mazingira awe na kitalu cha halmashauri maalumu lakini kwa bahati mbaya maafisa mazingira hawawezishwi hata milioni tatu kwa mwaka,” amesema Dkt. Jafo.
Aidha, waziri huyo amebainisha kuwa, bajeti hiyo ikitengwa kwa kila halmashauri itasaidia vijana waliokuwa katika halmashauri husika kupata shughuli za kufanya za kustawisha miche ambayo itanunuliwa na hivyo itasaidia kutengeneza ajira kwa vijana na hata urejeshaji wa mkopo wa
asilimia 10 utakuwa rahisi.