Naibu rais William Ruto wa Kenya, amemtaka Rais Uhuru Kenyatta kukumbuka vile amekuwa na urafiki naye wa karibu tangu mwaka 2002 wakati akiwania urais kwa mara ya kwanza.
Ruto alikuwa akizungumza kuhusu 2002 wakati Uhuru aliwania urais kwa mara ya kwanza chini ya tiketi ya chama cha Kanu.
“Rais Uhuru tunampenda ndio maana tulimchagua, Nilianza kumpigia kura Uhuru Kenyatta 2002, na kila wakati amesimama nimempigia kura kama rafiki yangu. Kama Uhuru ako na rafiki mkubwa Kenya hii ambaye amesimama na yeye anaitwa William Ruto,” aliongeza DP Ruto.
Hata hivyo, wakati huo Raila Odinga aliungana na Kibaki na kuunda muungano ambao ulizua wimbi la kisiasa la kumsomba Uhuru.
Kwa sasa, DP Ruto anahoji ni vipi Rais ameamua kumuunga Raila ilhali hajawahi kuwa rafiki wake kisiasa hapo awali.
“Ninataka nimwambie rafiki yangu Rais Uhuru Kenyatta, wacha kutuletea Raila . . . project kitendawili hatuwezi kuikubali. Sisi tunamuunga mkono Rais lakini project ya kitendawili haiwezekani Kenya, Wakenya miaka 20 iliyopita walikataa siasa za project. Kama walikataa wakati huo, ni saa hii karne ya 21 watakubali. Hatuwezi,” Ruto alimwambia Uhuru.
Wakati wa mkutano na wandani wake Musalia Mudavadi na Moses Wetangula eneo la Magharibi Ijumaa, Ruto alikuwa amemuonya Uhuru kuhusu kuleta siasa za project. Alimkumbusha namna Wakenya walimkataa 2002 kwa kuwa mradi wa aliyekuwa rais Moi na chama cha Kanu.
Katika mkutano wake wiki iliyoisha Rais Uhuru aliidhinisha urais wa Raila akisema taifa litakuwa katika mikono mizuri atakapoondoka mamlakani.
Huku akitetea uamuzi wake wa kushirikiana na kinara huyo wa ODM, Uhuru alisema kuwa alifanya mashauriano ya kina na nafsi yake huku akiongeza kwamba “yeye sio wazimu kumpuuza naibu wake.” “Mimi sio mwendawazimu eti niamke siku moja na kukaa na mtu ambaye nimemchukia karibu maisha yangu yote na nimpuuze naibu wangu mwenyewe. Je, mnadhani nilifikia uamuzi bila kuchunguza nafsi yangu? Nina sababu zangu na hivi karibuni nitawaambia Wakenya, lakini kwa wakati mwafaka,” Uhuru alisema.