Pimbi kwa kiingereza anaitwa Hyrax au rock burger, ni mnyama anayetajwa kuwa na harakati nyingi zisizo na maana na umachachari wake ulipelekea baadhi ya watu kupachikwa jina lake na hata kuna wakati wachora wa Katuni walitumia wahusika wa sanaa zao kwa kuwafananisha na mnyama huyu.

Ni jamii ya wanyama wenye maumbile madogo na vimo vifupi, ambao wanapatikana maeneo mbalimbali hasa barani Afrika na kutokana na maumbile yao madogo huwa ni vigumu sana kuwaona na bila kuwa makini unaweza zunguka bila kuwaona kwani huwa wana tabia ya kujificha.

Zipo jamii mbalimbali za Pimbi ambazo kwa utafiti inasemekana ni aina tatu, na mbili kati ya hizo ni wale wanaopatikana kwenye miamba na nyingine ni Pimbi wa kwenye miti ingawa wote hufanana kwa muonekano na ukubwa wa mwili.

MAISHA

Wanyama hawa, wana muonekano mfanano wa Mnyama mwingine mjanja zaidi aitwaye Sungura, kwani wana miguu mifupi, mikia mifupi na masikio ya duara. Sifa hizi zimepelekea wanyama hawa kupewa jina la Sungura wa kwenye miamba kwani wana fanana sana na Sungura.

Dume na jike huwa wana fanana kwa ukubwa na huwa ni vigumu kuweza kuwatofautisha ukiwa kwa mbali hivyo ili kuweza kuwatofautisha kati ya jike na dume lazima uweze kuwashika au kuwa karibu zaidi.

Pimbi ukiwachunguza vizuri katika nyayo za miguu na viganjani wana alama kama vitufe vyenye matezi mengi sana ya jasho, ambavyo huwasaidia wanyama hawa kuweza kukimbia na kushikilia kwenye miamba vizuri bila kupata athari au kuteleza.

Mbali na kuwa ni jamii ya wanyama wenye damu moto, lakini pimbi ni wanyama ambao wana uwezo mdogo sana wa kurekebisha jotoridi la mwili na kiasi kidogo sana cha mmeng’enyo wa chakula ukilinganisha za ukubwa wa miili yao.

Jotoridi katika miili yao hurekebisha kwa njia za kukusanyika pamoja, kukaa muda mrefu bila kufanya shughuli yoyote au wakati mwingine kwa kujitutumua. Hivyo kitu cha kwanza kukifanya asubuhi wanapo amka huwa wana lala kwenye miamba ili kupata joto.

Pimbi hawa huishi kwenye kundi ambalo huwa na kiongozi ambae ni dume mtawala hali ambayp ni tofauti na Pimbi wa kwenye miti ambao huishi kwa kujitenga, ila wale wa kwenye miamba huwa na uwezo wa kuona zaidi majira ya asubuhi na mchana tofauti na pimbi wa kwenye miti ambao wao wana uwezo wa kuona zaidi majira ya usiku.

Huwasiliana kwa njia ya sauti za miguno, mngurumo au kama filimbi na wakati huu kundi moja huweza kuliitikia kundi linguine popote walipo wa kiwa na urefu wa takribani Sentimeta 30 – 56, kimo cha Sentimeta 23 – 30 na uzito wa hadi Kilogramu 3 – 5.

CHAKULA

Chakula kikubwa cha wanyama hawa ni chenye asili ya mimea, japo kuna wakati mwingine wanyama hawa hula wadudu na baadhi ya viumbe jamii ya reptilian kama mijusi na hupendelea kula majira ya asubuhi kabla ya jua kuwa kali na tabia yao katika ulaji ni huwa kula kwa kutengeneza duara ili kuweza kuona pande zote kwa ajili ya kuwaepuka maadui zao.

Mara nyingi Pimbi hawa, hupendelea kula maeneo jirani na makazi yao, kwani huwa rahisi kukimbia na kujificha ndani ya miamba wakipendela sana majani, matunda, wadudu, mijusi na wakati mwingine mayai ya ndege, na hukaa muda mrefu bila kunywa maji kwani hupata maji yakutosha kupitia vyakula vyao.

KUZALIANA

Pimbi huzaa mara moja kwa mwaka na hupandana majira ya joto ambapo jike hubeba mimba kwa miezi saba / saba na nusu na ndiye mnyama mwenye umbo dogo ambaye hukaa na mimba kwa muda mrefu kulio wanyama wote wadogo Ulimwenguni, kisha huzaa majira ya kipupwe watoto 1-4 waliokamilia wakiweza kukimbia na kurukaruka baada ya muda mfupi usiozidi saa moja.

Watoto huwa chini ya uangalizi kwa miezi mitano na wote kwa pamoja wakike na kiume huwa tayari kwa kuzaa wafikishapo miezi 16 – 17 na wafikishapo umri wa miezi 16 – 17 watoto wa kike hujiunga na kundi la kina mama na wa kiume huanza kujiandaa kuondoka ndani ya kundi hilo kutokana na kufukuzwa na madume makongwe wakiwa hawajafikisha miaka mitatu na maisha yao Duniani ni miaka 8 – 12.

Maadui wakuu wa wanyama hawa ni Simba, Chui, Fisi, Mbweha, ndege Tai na nyoka hasa Chatu wa kwenye miamba na mpaka sasa bado hawajawa na tishio la binadamu kwa kiasi kikubwa kutokana na wengi wao kuishi maeneo tengefu ya uhifadhi wa wanyamapori hivyo wanakuwa na ulinzi wa kutosha.

HITIMISHO

Pimbi ni mnyamaa mpambanaji tu japo kidogo anaujinga ndani yake, kwani maisha yao yote huwa na ‘mishemishe’ zisizo na ratibaa maalum, yaani ‘wanapuyanga’ kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine lakini wakiwa hawana kitu cha kufanya wala plani na hapa ndipo ulizaliwa msemo wa ‘Harakati za Pimbi’.

Baadhi ya tafiti zinaonesha kuwa mkojo na kinyesi cha pimbi ni dawa kubwa sana ya ugonjwa wa Kifafa na pia inaarifiwa kuwa wana uwezo wa kula majani ambayo ni sumu kwa wanyama wengine na kuhusu harakati zao zisizo na faida inadaiwa kuwa anaweza kutoka mkuku kwenye pori moja kwenda jingine akifika huko analala halafu anarudi na hakuna alichoenda kufanya au kukiwahia kitendo kinachotafsiriwa kuwa ni kama kuamua kujichosha.⠀

Lakini pimbi wanamfumo wa kushangaza sana wa maisha yao, kwanza hutenga sehemu mbili tofauti za kujisaidia, yaani huwa kuna ‘washroom’ kwaajili ya haja ndogo na zile za haja kubwa na wote huwa wanaziheshimu sana hizi sehemu bila kuzingua na ule uwezo wa kula mimea yenye sumu pia huwasadia sana kwenye kuongeza spidi ya mmeng’enyo wa chakula tumboni.

Wataalamu wa Wanyama wanaarifu kuwa ukimuona Pimbi katulia kuwa makini usimguse kwani ni hatari sana maana anaweza kupunguza idadi ya vidole vya mkono wako.

CR Belouizdad yamng'oa Simon Msuva
Luis Miquissone amejitafuta, amejipata