Msanii wa Muziki wa Kizazi Kipya nchini Tanzania Rajab Abdul Kahali ‘Harmonize’ ametembelea Kambi ya Young Africans Avic Town Kigamboni jijini Dar es salaam, ili kuongeza hamasa kwa Wachezaji wa klabu hiyo kuelekea mchezo wa Jumapili (Oktoba 23) dhidi ya Simba SC.
Miamba hiyo itakutana Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku Mashabiki wa pande zote mbili wakitamba timu zao zinakwenda kuibuka na ushindi, ambao utaongeza alama tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Harmonize alionekana akiwa na wachezaji wa Young Africans jana Alhamis (Oktoba 20), walipokua kwenye mazoezi ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Simba SC, kwenye Uwanja wa Avic Town, Kigamboni.
Alipohojiwa kuhusu ziara yake kambini hapo, Msanii huyo alisema: “Nawatakia kila lakheri Wachezaji wote Kuelekea Mchezo wetu dhidi ya Simba SC. Mimi na familia Yangu ni mashabiki wa Young Africans na mara zote nimekuwa nikija uwanjani kuisapoti timu”
“Mimi naipenda sana Young Africans, nimetokea kwenye familia ambayo wote ni WANANCHI. Niwatakie kila la kheri kwenye mchezo wa Jumapili na mchezo wetu wa kimataifa”
“Young Africans ni jeshi kubwa, hatupaswi kukata tamaa kwa matokeo ya Sudan, bali inapaswa kuwa chachu au changamoto ya kupambana maradufu zaidi”
“Najua wengi wetu wamefadhaika na matokeo, lakini kumbukeni mwanajeshi hakati tamaa akiangushwa chini. Hii ni ishara ya kujifunza pale ambapo tumeanguka. Nafasi bado ipo, sababu tunazo, nguvu tunayo”