Klabu ya Manchester United imejipanga kumsajili Mshambuliaji kutoka England na Klabu ya Tottenham, Harry Kane mwishoni mwa msimu huu, ili kuboresha kikosi chao, kuelekea msimu ujao wa 2023/24.
Taarifa zinaeleza kuwa Uongozi wa Manchester United umepanga kufanya hivyo huku ikijiandaa kukwepa mgogoro ambao huenda ukajitokeza kati yao na Uongozi wa Tottenham ambao haupo tayari kumwachia.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 29 amebakiza zaidi ya mwaka mmoja katika mkataba wake, na anaweza kuruhusiwa kuondoka msimu huu wa joto huku Erik ten Hag akitaka kuongeza Mshambuliaji wa kiwango cha Dunia kwenye kikosi chake cha United.
Iwapo mwenyekiti wa Spurs Daniel Levy ataikataa ofa inayoandaliwa huko Old Trafford, United wanaweza hata wasijihusishe na kutafuta washambuliaji wengine badala yake, huku mshambuliaji wa Napoli, Victor Osimhen pia akihusishwa na kuhamia Man utd.
Nyota huyo wa Nigeria amefunga mabao 21 katika michezo 27 ya michuano yote msimu huu na kuisaidia timu yake ya Napoli kusonga mbele kwa alama 18 kileleni mwa Serie A kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Atalanta Jumamosi iliyopita.
United wanaweza kukabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa klabu kadhaa za zinazoshiriki Ligi Kuu ya England (Premier League) na Ulaya ikiwa watajaribu kumsajili Osimhen, huku Chelsea, Arsenal na Paris Saint-Germain zikiwa miongoni mwa kundi linalowinda saini yake.