Klabu ya Manchester United imeripotiwa kuwa kwenye mazungumzo na staa wa Bayer 04 Leverkusen ya Ujerumani, Jeremie Frimpong wakati huu wakiwa na mpango wa kupiga bei mabeki wao wengi kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya.
Frimpong mwenye umri wa miaka 22, ni beki wa kulia ambaye amemvutia kocha Erik ten Hag kwenye harakati zake za kusaka mtu wa maana wa kwenda kucheza kwenye nafasi hiyo.
Ripoti zinafichua kwamba Man United wamejiandaa kusikiliza ofa za kumhusu beki wa kulia Aaron Wan Bissaka kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi, huku beki mwengine Diogo Dalot, ambaye atakuwa huru mwisho wa msimu amekuwa kwenye rada za timu nyingi kama Juventus, FC Barcelona, Atletico Madrid na AC Milan.
Mabeki hao wote wameripotiwa watafunguliwa mlango wa kutokea kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi huku Ten Hag akiwa na mpango wa kuuza mabeki wa pembeni wasiopungua watatu.
Na hawatakuwa mabeki wa pembeni tu, bali kocha huyo Mdachi amepanga kufanya mabadiliko makubwa kwenye safu yake ya ulinzi. Phil Jones, ambaye pia mkataba wake utakwisha Juni mwaka huu, atafunguliwa mlango wa kutokea, sambamba na nahodha Harry Maguire, ambaye pia anauzwa, huku Paris Saint-Germain ikipanga kutumia Pauni 50 milioni kunasa saini yake.
Man United ina mpango pia wa kuwaacha Eric Bailly, Alex Telles na Brandon Williams.
Na kuziba pengo la hao watakaoondoka, tayari Ten Hag ameshaanza mchakato wa kumleta Frimpong, mchezaji ambaye aliibukia kwenye akademia za Manchester City kabla ya kwenye Celtic mwaka 2019.
Kisha alihamia Leverkusen miaka miwili iliyopita na tangu hapo amekuwa panga pangua kwenye kikosi cha Uholanzi, ambapo alijumuishwa kwenye kikosi cha Kombe la Dunia 2022 fainali zilizofanyika Qatar.
Sambamba kuboresha safu ya ulinzi, kocha Ten Hag anahitaji straika mpya pia na kwenye mipango na rada zake amewaweka Harry Kane wa Tottenham na Victor Osimhen wa SSC Napoli.