Wakati majogoo wa jiji la Liverpool wakijiandaa kumpa ofa tamu beki wao kutoka nchini Uholanzi, Virgil van Dijk ambayo itamuewesha kulipwa mshahara mnono, inadaiwa kuwa beki wa Manchester United, Harry Maguire amekua kichocheo kikubwa cha kufanikisha jambo hilo.
Man United iliweka rekodi ya kumsajili Maguire kwa dau kubwa la Pauni milioni 80 wakati wa majira ya kiangazi, akitokea Leicester City FC, aliyoitumikia tangu mwaka 2017.
Uhamisho huo ulimfanya Maguire ampiku Van Dijk, ambaye awali aliweka rekodi ya kuwa beki ghali zaidi duniani, kufuatia uhamisho wake kuigharimu Liverpool Pauni milioni 75, akitokea Southampton FC mwaka 2018.
Mkataba wa sasa wa beki huyo anayeshikilia taji la mchezaji bora wa mwaka wa barani Ulaya umesaliwa na muda wa miaka minne, huku akilipwa mshaha wa Pauni 125,000 kwa juma.
Taarifa kutoka Anfield zinaeleza kuwa, dili lililowekwa mezani kwa ajili ya Van Dijk, litamuwezesha kulipwa mshahara wa Pauni 200,000 kwa juma, huku akitarajiwa kusaini mkataba wa miaka miwili, ambao utamfanya kusalia klabuni hapo kwa miaka sita ijayo.
Van Dijk alikuwa mchezaji muhimu wakati Liverpool iliponyakua taji lao la sita la Ulaya na mwaka huu, anapewa nafasi kubwa ya kubeba tuzo ya mchezaji bora wa dunia 2019 (Ballon d’Or), akishindanishwa na Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.