Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Simba SC Hassan Dalali amemshauri Mwenyekiti wa sasa wa Klabu hiyo Murtaza Mangungu kwa kumtaka ajitafakari na kuitafakari Klabu hiyo kwa ujumla.

Dalali ameibuka na kutoa ushauri huo, kufuatia makandokando yanatotajwa kuwa chanzo cha Simba SC kusuasua katika michezo yake ya hivi karibuni, ikipoteza michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuambulia sare dhidi ya Azam FC katika Ligi Kuu.

Mzee huyo amesema amesikia tofauti zilizozalishwa na matokeo ya Uchaguzi Mkuu, zimekuwa chachu ya kufanya vibaya kwa timu yao, hivyo Mangungu anapaswa kusimamia kauli yake ya kuvunja makundi baada ya Uchaguzi kwa vitendo.

“Binafsi baada ya uchaguzi kila kitu nilikiweka kando, naipenda Simba SC natamani ifanye makubwa, siwezi kuchochea makundi ndani ya klabu na kama wanaofanya hivyo wanafanya kwa faida ipi!”

“Japokuwa baada ya uchaguzi Mangungu alisema uchaguzi umepita sasa tujenge Simba moja, ila ni bora angeitisha mkutano ili kujadili mambo mbalimbali ya afya kwa klabu, kwani atapata picha nzima ya mitazamo ya watu anaowaongoza.” amesema Dalali

Mangungu alitangazwa kuwa Mwenyekiti wa Simba SC kwa ushindi wa Kura 1311 dhidi ya mpinzani wake Adv. Moses Kaluwa aliyepata kura 1045.

Kwa ushindi huo Mangungu alipata wasaa wa kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Simba SC kwa kipindi cha miaka minne ijayo, baada ya kuiongoza Klabu hiyo kwa miaka miwili tangu 2021.

Kwa upande wa Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi walioshinda ni Dr Seif Ramadhan Muba (1636), Asha Baraka (1564), CPA Issa Masoud Iddi (1285), Rodney Chiduo (1267) na Seleman Harubu (1250).

Jumla ya Wanachama Simba SC waliopiga Kura ni 2363 Kura halali, lakini Kura halali zilikuwa 2356.

Tanzania inakwama kwa mambo matano: Kitwanga
Wapeni watoto nafasi watimize ndoto zao: RC Telack