Kiungo Mshambuliaji Hassan Dilunga amesema hana budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa hali anayoipitia kwa sasa, huku akiachwa kwenye kikosi cha Simba SC.
Dilunga hakuwa sehemu ya Wachezaji wa Simba SC waliotambulishwa rasmi kwa ajili ya msimu huu 2022/23 katika Tamasha la Simba Day, kutokana na kusumbuliwa na jeraha la goti tangu msimu uliopita.
Akizungumza Dar es salaam, Kiungo huyo amesema anaamini anayoyapitia kwa sasa ni sehemu ya ibada kwa mujibu wa imani ya dini yale ya kiislamu, hivyo hana budi kumshukuru Mwenyezi Mungu.
Amesema kwa sasa bado yupo chini ya uangalizi wa Madaktari, lakini anaendelea na mazoezi mepesi, ambayo ni sehemu ya tiba itakayomuwezesha kurejea Uwanjani kwa haraka, baada ya kuwa nje kwa miezi kadhaa.
“Mashabiki wasidhani kama nipo katika wakati ngumu sana, binafsi kwa imani yangu ninaamini nipo kwenye ibada, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa hili,”
“Kwa sasa nipo chini ya Ungalizi wa madaktari na ninafanya mazoezi kwa mujibu wa maagizo yao, naamini hiki ninachokifanya kitaniwezesha kurejea katika hali yangu kama ya zamani na nitacheza tena soka In Shaa Allah.” amesema Dilunga
Dilunga alikua sehemu ya kikosi cha Simba SC kilichopata mafanikio kwa kutwaa Ubingwa wa Tanzania Bara mara nne mfululizo, Kombe la Shirikisho mara mbili na kufika hatua ya Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu wa 2018/19 na 2020/21.
Msimu uliopita Dilunga alifanikiwa kuipeleka Simba SC hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kufunga bao la kufutia machozi dhidi ya Red Arrows ya Zambia iliyoshinda nyumbani 2-1, lakini awali ilipokea kisago cha 3-0 kwenye mchezo uliopigwa jijini Dar es salaam