Uongozi wa Klabu ya Simba SC umeingia mkataba wa miaka miwili na Kampuni ya Bima ya Afya ya Mo Assurance, wenye thamani ya Shilingi Milioni 250 kwa mwaka.

Bima hiyo itakayohusika kwa timu zote tatu za Simba SC kwa maana ya timu kubwa, timu ya Wanawake na Ile ya vijana, pia itawafikia waajiriwa wote wa Klabu hiyo na familia zao, ambapo kila mmoja atakuwa na nafasi ya kuongeza watu wanne tegemezi kwenye bima hiyo ambao ni mke/mume na watoto.

Akizungumza katika hafla ya kusaini mkataba huo leo Ijumaa (Oktoba 28) jijini Dar es salaam, Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Barbara Gonzalez ameeleza namna timu hiyo itakavyonufaika na mkataba huo.

“Tumekuwa tukitumia gharama kubwa kwenye matibabu ya wachezaji na waajiriwa wengine wa Simba lakini ujio wa bima hii utatusaidia kwenye gharama hizo nakuongeza ufanisi kwa kila mtu kwenye eneo lake,” amesema Barbara.

Mkurugenzi wa Masoko wa kampuni ya Mo Assurance, Fatema Dewji amesema mkataba huo umesainiwa baada ya majadiliano ya muda mrefu huku akiamini utakuwa msaada kwa Simba na kampuni yake.
“Pande zote mbili tumejadili kwa muda mrefu kuhusu mkataba huu na Sasa tumesaini.

“Utasaidia katika matibabu na kuwafanya Wachezaji na waajiriwa wengine wa Simba kutowaza Tena suala la matibabu na kutimiza majukumu yao kwa kujiamini zaidi,” amesema Fatema.

Huduma ya Bima hiyo inapatikana kwenye hospitali zote kubwa nchini na itatumika kwa matibabu ya kawaida, kulazwa na majeraha yanayotokea mchezoni.

Korea kumuunga mkono Rais Samia ujenzi Chuo cha TEHAMA
Kamisaa wa Sensa Balozi Hamza: Matokeo ya sensa tayari