Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Ardhi Lusajo Mawakabuku amesema kuwa hati miliki za ardhi zitatolewa ndani ya siku moja kwa wananchi aliokamilisha taratibu za kupatiwa hati wakati wa Maonyesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba
Amebainisha hayo wakati akieleza mipango mikakati ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika ushiriki wa maonyesho ya Sabasaba yanayofanyika viwanja vya Mwl. Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Amesema kwa mwaka huu kwenye maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) Wizara imejipanga vizuri kuhakikisha inatoa na kutangaza huduma zinazotolewa ili kukidhi kiu wa wananchi watakaotembelea Banda la Wizara ya Ardhi.
Mwakabuku amesema nyaraka zinazotakiwa kwa mmiliki wa kiwanja anayetaka kupatiwa hati ni michoro ya mipango miji, ramani ya upimaji, fomu ya majirani , kitambulisho cha uraia pamoja na barua ya maombi.
Kupitia maonesho hayo ya Sabasaba Mwakabuku alisema, wananchi wataweza pia kununua ramani zenye wilaya mpya za Tanzania sambamba na wale wenye migogoro ya ardhi kuweza kuwasiliana moja kwa moja na makamishna wa ardhi wasaidizi wa mikoa ili kupata ufumbuzi wa migogoro katika maeneo yao.
Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanaanza rasmi siku ya jumatatu tarehe 28 Juni 2021 na kumalizika Julai 10, 2021 ambapo kauli mbiu ya maonesho hayo kwa mwaka huu wa 2021 ni Uchumi wa Viwanda kwa Ajira na Biashara Endelevu.