Jopo la wajumbe maalumu lenye nguvu ya kumchagua rais wa Marekani, maarufu kama Electoral College limemthibitisha Joe Biden kuwa Rais ajae wa urais wa taifa hilo.
Biden amesema kuwa utashi wa watu umeshinda baada ya ushindi wake wa uchaguzi kuthibitiswa na wajumbe hao
Katika hotuba aliyoitoa baada ya kutangazwa kwa ushindi huo Biden amesema kuwa demokrasia ya Marekani imesukumwa na kujaribiwa na imedhihirisha kuwa ni jasiri ya kweli na thabiti.
Hata hivyo hatua ya uthibitisho kwa Biden inatajwa kuifunga milango kwa mpinzani wake Donald Trump katika jitihada zake za kisheria za kuyageuza matokeo ya uchaguzi wa 2020.
Pia kuthibitishwa kwa ushindi huo ni mojawapo ya hatua alizohitaji Biden ili kumuwezesha kuchukua mamlaka ya urais.
Hatua hiyo inafanyika huku mteule huyo akimkosoa mpinzani wake huyo kwa maneno makali tangu kumalizika kwa uchaguzi kwa kumwita mpinga matakwa ya umma na mkaidi Katiba ya nchi.