Wakuu wa kijeshi wa jumuiya ya Afrika Magharibi ECOWAS watakutana Alhamisi na Ijumaa nchini Ghana kujadili uwezekano wa kuingilia kijeshi nchini Niger bada ya hapo awali kuahirishwa kutokana na sababu walizodai kuwa ni za kiufundi.
Hata hivyo, nchi jirani za Mali na Burkina Faso zimetishia uingiliaji wowote wa kijeshi nchini Niger itakuwa tangazo la vita huku Urusi ikionya kuwa uingiliaji huo wa kijeshi unaweza kusababisha vurumai za muda mrefu na kushindwa kupata amani ya moja kwa moja ya Taifa hilo.
Kiongozi wa kijeshi wa Mali, Kanali Assimi Goita alisema amezungumza kwa simu na Rais wa Urusi Vladimir Putin kuhusu hali ya Niger, ambapo kiongozi huyo wa Urusi alisisitiza umuhimu wa kutatua kwa amani kwa njia zilizo salama kwa maslahi ya eneo la Sahel yenye hali utulivu zaidi.
Jumamosi iliyopita (Agosti 12, 2023), Viongozi wa Mapinduzi ya Kijeshi wa Niger walisema wako tayari kuzingatia mazungumzo ya kidiplomasia na ECOWAS, kufuatia mizozo kadhaa na wajumbe wa kikanda na Kimataifa, ambao walijaribu kupatanisha mgogoro wa kisiasa nchini humo.