Kiungo mshambuliaji kutoka nchini Ubelgiji na klabu ya Manchester City Kevin de Bruyne, huenda akarejea uwanjani kesho jumapili, wakati wa mchezo wa ligi kuu ya England dhidi ya wenyeji Liverpool.
De Bruyne, anapewa nafasi ya kurejea kwenye mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka duniani kote, baada ya kuonyesha yupo tayari kiafya, kufuatia mazoezi aliyoyafanya siku za karibuni.
Taarifa za awali zilieleza kuwa, kiungo huyo alikua anatarajiwa kurejea uwanjani mwishoni mwa mwezi Oktoba ama mwanzoni mwa mwezi Novemba, kufuatia ukubwa wa jeraha la goti alilolipata mwezi Agosti.
Meneja wa Man City Pep Guardiola, amewaambia waandishi wa habari kuwa, uwezekano wa kumtumia De Bruyne katika mchezo huo wa kesho, utategemea na majibu vipimo vya mwisho atakavyofanyiwa leo jumamosi.
“Tunaendelea kusubiri majibu ya vipimo atakavyofanyiwa, kama madaktari watanipa ruhusa ya kumtumia, nitafanya hivyo.”
“Amekua na maendeleo mazuri tangu alipoanza mazoezi mepesi majuma mawili yaliyopita, kila mmoja alishangazwa na uharaka wa kurejea kwake, lakini bado ninasisitiza majibu ya vipimo vya leo yatakua suluhisho la kutumika dhidi ya Liverpool, ama kuendelea kukaa nje.” Alisema meneja huyo kutoka nchini Hispania.
Katika hatua nyingine beki wa kushoto wa mabingwa hao wa soka nchini England Benjamin Mendy, anatarajiwa kurejea kikosini kesho jumapili kuwakabili Liverpool, baada ya kukosa michezo sita, kufuatia majeraha ya mguu.
“Kila mmoja yupo tayari kwa mchezo wetu dhidi ya Liverpool, lakini Delph hatoakua sehemu ya kikosi, Gundogan ana nafasi finyu ya kucheza kutokana na kushindwa kufanya mazoezi kwa siku kadhaa, naye atafanyiwa vipimo ili kujua maendeleo yake.”