Imeelezwa kuwa asilimia 48 ya wanafunzi wa kike wanakosa masomo kutokana na kuwa katika mzunguko wa hedhi hali ambayo huathiri uwezo wa wanafunzi hao kujifunza kwa ufasaha.

Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Waziri wa afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati akifungua warsha ya usambazaji matokeo ya utafiti juu ya hedhi salama uliofanyika kwa wanafunzi wa kike katika mikoa 16 nchini.

Waziri ummy utafiti huo uliofanywa mwaka 2015 na shirika la SNV Netherlands Development pamoja na Tanzania Water and Sanitation Network (TAWASANET) katika halmashauri za Sengerema, Mufindi, Chato, na Temeke ulionesha kuwa asilimia 48 ya wanafunzi wa kike hukosa masomo wanapokua kwenye hedhi asilimia 78 ya waliohojiwa walisema kipindi cha hedhi huathiri uwezo wao wa kujifunza.

“Ikumbukwe katika kipindi cha kupevuka mabinti, vijana walio shule hupitia kipindi cha mabadiliko ya ukuaji yani balehe, hivyo kipindi hiki ni muda muafaka wa kutoa elimu kwa Watoto, kujenga misingi ya maadili na misingi ya afya bora”. Amesema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amesema kupitia utekelezaji wa kampeni ya taifa ya usafi wa mazingira kupitia program endelevu yam aji na usafi wa mazingira vijijini yam waka 2020/21, Serikali imeweza kujenga miundombinu ya vyoo vikiwemo vya wanafunzi wenye ulemavu pamoja na sehemu ya hedhi salama ambayo ina vifaa muhimu vinavyohitajika katika shule 835 kwenye mikoa 17 na halmashauri 86.

Waziri Ummy Mwalimu katika picha ya pamoja na wadau wa masuala ya Hedhi salama

Kupitia taarifa iliyotolewa na ofisi ya taifa ya takwimu (NBS) juu ya masuala ya maji na usafi mazingira shuleni ya mwaka 2018 inaonesha asilimia 66.8 ya shule ndizo zina huduma ya hedhi salama ambapo kati ya hizo zilizobainika kuwa na viteketezi ni asilimia 24 huku asilimia 22.8 zinatupa taka kwenye mashimo na 19.5 zina vichomea taka visivyokidhi.

Waziri Ummy amesema pamoja na jitihada za Serikali na wadau bado tatizo la hedhi salama shuleni ni pana na linahitaji mikakati endelevu, hivyo serikali iliona kuna haja ya kufanyia utafiti.

Waziri Ummy ameipongeza taasisi ya taifa ya utafiti wa magonjwa ya binadamu kwa kushirikiana na maabara ya afya ya jamii Pemba kwa utafiti huo ambao umeshrikisha mikoa 19 ikiwemo miwili ya Tanzania visiwani na kufikia shule 294 na kuwahusisha washiriki Zaidi ya 10,000 watoto wa shule, walimu, wazazi, viongozi wa jamii na viongozi wa halmashauri na kitaifa.

Tanzia: Msanii Maunda Zorro afariki dunia
Habari kubwa kwenye magazeti leo, April 14, 2022