Hatimaye mabingwa wa soka nchini Italia, Juventus FC wamekamilisha azma ya kumrejesha kikosini beki kisiki Leonardo Bonucci, akitokea kwa wababe wa mjini Milan, AC Milan.
Juventus wamefanikisha azma hiyo, baada ya mshambuliaji Gonzalo Higuain na beki Mattia Caldara kutolewa kama sehemu ya makubaliano ya uhamisho wa Bonucci kurejea Juventus.
Tayari Gonzalo Higuain na Mattia Caldara wameshakamilisha mpango wa kujiunga na AC Milan baada ya kufanyiwa vipimo vya afya jana Alkhamis, sambamba na mambo mengine ya msingi ambayo yanawafanya kuanza harakati za maisha mapya mjini Milan.
Hata hivyo, taarifa zilizotolewa usiku wa kuamki leo na uongozi wa AC Milan zimeeleza kuwa Higuain mwenye umri wa miaka 30 amejiunga na klabu hiyo kwa mkopo, huku Caldara mwenye umri wa miaka 24 akisajiliwa jumla.
Caldara amesaini mkataba wa miaka mitano, kwa mujibu wa AC Milan.
Gonzalo Higuain
Mattia Caldara
Kwa upande wa Juventus, wanatarajiwa kumtangaza rasmi Bonucci leo Ijumaa katika mkutano na waandishi wa habari.
Beki huyo anarejea Juventus, kuendeleza harakati za kuitumikia klabu hiyo ambayo tayari alikua ameshaichezea katika michezo 319 kabla ya kuondoka mwaka 2017.