Mshambuliaji wa Coastal Union Hija Ugando amesema alijitahidi sana kutafuta nafasi ya kucheza soka nje ya nchi lakini wakala wake alikuwa akimpeleka timu kubwa kuliko uwezo wake.
Ugando alipata fursa ya kufanya majaribio Club Sporting Sfaxien ya Tunisia na vikosi B na C vya Atalanta ya Italia lakini anasema vilabu hivyo vilikuwa vikubwa sana ukilinganisha na uwezo wake.
“Mambo hayakwenda vizuri Sfaxien ni timu kubwa sana ilichukua ubingwa wa Champions League Africa mwaka 2012 kwa hiyo ilikuwa ngumu sana kwangu, nikashindwa.”
“Wakala akaniambia ameona nina uwezo mkubwa inabidi anipeleke timu ndogo inayoendana na uwezo wangu. Akafatilia na kupata timu Italia Atlanta, nikaenda lakini Atalanta ni kubwa kuliko hata hiyo niliyoshindwa Afrika kwa hiyo ikawa ngumu pia.”
Ugando amewahi kucheza Simba lakini hakudumu akaondoka, anasema aliomba mwenyewe kuondoka Simba.
“Ukiwa kijana ndio unaanza mambo mengi yanakukuta uzoefu huna, hujazoea mazingira, timu ina presha ya ubingwa.”
“Simba yetu ilikuwa inapigana kupata ubingwa baada ya kuukosa kwa muda mrefu kwa hiyo kulikuwa na presha kubwa. Kwa kijana kuanza kucheza inakuwa ngumu.”
“Hata kocha anakupa nafasi anapoona kuna mazingira rahisi kwako kwa sababu watu sio wavumilivu kwa hiyo hawezi kukupanga kila mara kutokana na uzoefu ulionao.”
“Nilikaa Simba kwa msimu mmoja na nusu nikaona nafasi imekuwa ngumu, nikaomba mwenyewe kuvunja mkataba baaada ya kuona siwezi kutumika.”
Hija Ugando ametoka wapi?
Maisha yake ya soka yalianza kwenye Copa CocaCola 2010 akiwa na timu ya Kinondoni ambayo ilitolewa hatua ya robo fainali kwa mikwaju ya penati lakini yeye alikuwa miongoni mwa wachezaji waliochaguliwa na kujiunga kwenye academy ya Azam FC.
Kwenye academy ya Azam FC mambo hayakuwa mazuri sana kwa sababu hakukaa sana akaondoka na kujiunga na kituo cha Jack Football Academy-Mbagala.
Mwaka 2014 alienda Kenya kufanya majaribio akiwa na wenzake watatu lakini alifuzu pekeake wengine walifeli. Akacheza ligi kuu kama miezi sita (6) hivi ile timu ikashuka daraja (yeye alisajiliwa dirisha dogo). Akarudi Bongo na kuanza kutafuta fursa za kucheza nje ya nchi, akapata Tunisia na Italia.