Ni siku chache tu zimepita tangu Rais wa kwanza wa Zambia, Kenneth Kaunda afariki dunia akiwa na umri wa miaka 97.
Ameondoka duniani na kuacha vitu vingi vya kukumbukwa, lakini leo acha nikupe hili la mavazi, amefariki akiacha jina maarufu la kaunda suti, ambazo kwa sasa vijana, watoto na wazee wanavaa na kupendeza.
Miaka ya 1920 wabunifu wawili kutoka nchini ufaransa ted lapidus na yves st laurent walibuni safari suits ambazo lengo ilikuwa ni kusafiria kutoka nchi za ulaya kwenda nchi za Afrika.
Safari Suits zilikuwa hazina nafasi ya kuweka tai na zilikuwa zinatengenezwa kwa pamba nyepesi zinazohimili hali ya hewa ya joto na zilikuwa na mifuko mingi ili kumuwezesha msafiri kuweka vyakula pamoja na chupa za maji ya kunywa.
Safari Suits pia zilitumiwa na jeshi la british na kuwekwa nyota katika zile kola pana.
Aidha mnamo miaka ya 1960 ulizuka ushindani mkubwa wa mavazi kwa mataifa ya Afrika ambapo marais walikuwa wanapambana kuonyesha ubunifu wa vazi litakalotambulisha taifa.
Hayati baba wa taifa, Mwl Julius Nyerere aliasisi vazi lake lisilokuwa na kola(rejea mavazi anayovaa mzee malecela), kwame nkurumah wa ghana aliasisi vazi la blanketi ambalo alikuwa anajifunika kama mgolole hivi.
Kaunda wa zambia akajikita katika vazi la safari suit ambalo likampa umaarufu afrika nzima na hadi leo bado tumebaki na jina hilo la kaunda suti.
Jina kaunda suit limeua jina la safari suit, kwa sasa zipo aina nyingi za kaunda suti ambazo zinashonwa kwa ustadi wa hali ya juu, pumzika kwa amani Mzee Kaunda.