Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka amesema Serikali imedhamiria kufunga kamera za usalama katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma kwa lengo la kupunguza uhalifu ambao umeanza kushamiri katika maeneo ya jiji hilo baada ya Serikali kuhamia Dodoma.

Akizungumza leo Juni 19, 2021 wakati wa Hafla ya kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Kituo cha Polisi Chang’ombe kinachojengwa katika eneo la Chang’ombe, jijini Dodoma, RC Mataka amesema hali hiyo imejitokeza kutokana na wingi wa watu mkoani hapo.

“Maeneo mengi ya jiji la Dodoma tutafunga kamera za usalama barabarani, hatuwezi kuwa na jiji ambalo  polisi wetu wanakimbizana na wahalifu muda wote, tutatumia teknolojia hiyo kudhibiti uhalifu wa aina mbalimbali, Dodoma ni Makao Makuu ya nchi lazima pawe salama nawashauri wahalifu watafute shughuli nyingine ya kufanya hapa si salama tena kwa kazi zao,” Amesema Mtaka.

Aidha adhma hiyo ya kujenga kituo imekuja baada ya matendo ya uhalifu ikiwemo uporaji, ubakaji, udhalilishaji, matumizi ya dawa za kulevya kushamiri katika maeneo ya Chang’ombe hali inayopelekea wananchi wa maeneo hayo kuishi kwa wasiwasi wakihofia matendo hayo ya uhalifu.

Amesema kuwa kwa eneo la Chang’ombe mkoani Dodoma linakua kwa kasi hivyo linahitaji kituo cha polisi kitakachokuwa kinafanya kazi masaa 24

Akizungumza kwa niaba ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Naibu Katibu Mkuu Ramadhani Kailima amesema wizara imetoa kiasi cha shilingi milioni 10/= kama mchango wake katika ujenzi wa kituo hicho na kikikamilika  kitaweza kutoa huduma mbalimbali ikiwemo upelelezi wa matukio, upelekaji wa majarada ya kesi kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ambayo yatapelekwa mahakamani kwa hatua za kisheria.

Hiki ndo chanzo cha Kaunda Suit
Afisa ugani wakumbushwa kauli ya Majaliwa