Kiungo wa klabu bingwa Afrika mashariki na kati Azam FC, Himid Mao Mkami ameondoka nchini usiku wa kuamkia leo kuelekea nchini Denmark, kwa ajili ya kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa kwenye klabu ya Randers FC inayoshiriki ligi kuu ya nchi hiyo maarufu kama Danish Superliga.
Himid, 24, atakuwa Randers kwa majaribio ya kipindi cha siku kumi (10) kisha atarejea nchini na kuendelea na majukumu ndani ya kikosi cha Azam FC.
Randers FC ilianzishwa Januari mosi, 2003 na hucheza michezo yake ya nyumbani kwenye uwanja wa Auto C Park Randers wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 11,000.
Mei 11, 2006, Randers FC iliweka rekodi baada ya kuchukua ubingwa wa kombe la ligi ya Denmark (Danish Cup), kwa kuichapa Esbjerg bao 1-0 kwenye mchezo wa fainali uliochezwa kwenye uwanja wa Parken Stadium. Wakati huo Randers FC ilikuwa ligi daraja la kwanza.