Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeahidi kushughulikia suala la huduma za afya bure kwa watu wenye ulemavu.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamisi Andrea Kigwangalla leo Bungeni Mjini Dodoma kwa niaba ya Waziri Ummy Mwalimu.

Dkt. Kigwangalla amesema hayo wakati wa kipindi cha maswali na majibu kufuatia swali la Mbunge wa Viti Maalum Stella Ikupa Alex aliyetaka kupata ufafanuzi juu ya suala hilo.

Dkt. Kigwangalla amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kutoa huduma za afya bure kwa makundi maalum likiwemo watu wenye ulemavu.

“Dhumuni la Sera ya Afya ya mwaka 2007 ni kuwezesha watu wenye ulemavu wazingatiwe katika makundi maalum ya watu wanaostahili msamaha utolewao kwa kuzingatia endapo mlemavu huyo hana uwezo wa kulipia huduma hiyo au awe katika makundi maalum ili kupata huduma bora za afya kama ilivyo kwa watu wengine,” alisisitiza Dkt. Kigwangalla.

Sera hiyo imeainisha makundi maalum yanayostahili kupata msamaha wa huduma za afya katika vituo vyote vya kutolea huduma kuwa ni wazee wenye umri zaidi ya miaka 60, watoto chini ya miaka mitano,watoto waishio katika mazingira hatarishi, wajawazito na watu wasiojiweza kiuchumi.

Dkt. Kigwangalla amesema kuwa watu wengine ambao wapo kwenye makundi maalumu ni wenye magonjwa sugu kama  Kifua kikuu, Ukimwi, Kisukari, Magonjwa ya Moyo, Pumu, Sikoseli, Ukoma, Saratani na Magonjwa ya Akili.

Katika kuweka uwiano sawa kwa Watanzania wote bila ubaguzi, Dkt. Kigwangalla amesema Serikali ya awamu ya tano ina pendekezo la kutoa bima ya afya ya lazima kwa watu wote ambapo utasaidia pia kwa watu wenye msamaha kupata huduma bora.

Kama Serikali itapitisha pendekezo la kutoa bima ya afya ya lazima kwa Watanzania wote litasaidia upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.

Mbao Waivutia Kasi Azam FC
Himid Mao Kujaribu Soka Ulaya