Mwandishi wa habari za michezo mwandamizi Edo Kumwembe amefunguka kuhusu usajili wa wachezaji unaoendelea kwa sasa kwa klabu kubwa za Simba SC, Young Africans na Azam FC.
Klabu hizo tatu zimetumia ukubwa wao wa majina na kiuwezo wa fedha kufanya usajili wa nguvu, ambao unaaminika utazisaidia kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya Kimataifa.
Edo ambaye pia ni Mchambuzi wa Soka la Bongo amefunguka kuhusu usajili wa klabu hizo, huku akionesha kushangazwa na ujio wa wachezaji wengi kutoka nchi jirani na Tanzania hususan DR Congo, tofauti na ilivyokua misimu iliyopita.
Young Africans imekua klabu pekee kwa sasa, kwa kuwasajili asilimia kubwa ya wachezaji kutoka DR Congo, baada ya kufanya hivyo msimu uliopita ikiwasajili Tuisila Kisinda na Mukoko Tonombe waliopishana na Papii Kabamba Tshishimbi na David Molinga.
Edo amesema: Wachezaji kutoka DR Congo wana maarifa uwanjani. Kifupi ni kwamba wana vipaji. Lakini hata sisi si tuna vipaji? Ndio, tena vikubwa. Wachezaji karibu wote wa Tanzania wana vipaji. Tofauti ni kwamba juu ya vipaji vya wachezaji wetu Wakongo wao wameongeza matumizi ya nguvu.
Ni kitu ambacho kitawatofautisha wachezaji wetu na wale wa nje kwa muda mrefu.
Sijui tunakosea wapi lakini ukweli ni kwamba licha ya ubishoo wao nje ya uwanja lakini wachezaji wa DR Congo wana matumizi makubwa ya nguvu na wanapania wanapocheza soka. Congo haina wachezaji legelege.
Nje ya uwanja wachezaji wa DR Congo ni mabishoo. Wanapenda kuvaa hereni, kusuka nywele, kuongeza rangi katika miili yao na mengineyo.
Wakiingia uwanjani wanapiga kazi kuliko wachezaji wetu ambao wengi wao ni legelege. Sielewi tatizo linaanzia wapi. Ndivyo tulivyozaliwa? Hapana.
Zamani tulikuwa na kizazi cha kina Athuman China na wengineo. Walikuwa wana vipaji vikubwa vya mpira lakini matumizi yao ya nguvu pia yalikuwa juu.
Leo wachezaji wenye matumizi ya nguvu nchini wamepotea. Wengi wamebakiza vipaji tu.