Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC wapo kwenye hatua nzuri ya kumalizana na Mshambuliaji kutoka nchini Ghana, Abdul Basit Khalid aliyeachana na klabu ya Esperance ya Tunisia.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba SC iliyowasili jana Jumatano (Agosti 11) nchini Morocco, kwa ajili ya kuweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu na Michuano ya Kimataifa zinaeleza kuwa, Mshambuliaji huyo atajiunga na kikosi cha Mabingwa hao mjini Casablanca endapo dili lake litakamilishwa kama inavyotarajiwa.

Mshambuliaji huyo machachari ndiye anayepewa nafasi kubwa na benchi la ufundi ingawa pia Mshambuliaji kutoka DR Congo, Kadima Kabangu nae ameshakubaliana mambo mengi na viongozi wa Mabingwa hao wa Tanzania bara na wamemwambia akae mkao wa safari.

Kocha Mkuu wa Simba SC Didier Gomes ambaye ni raia wa Ufaransa, anaukubali zaidi aina ya uchezaji wa Khalid na uzoefu wake kimataifa, jambo ambalo linaweza kuwabeba Simba SC msimu ujao unaotarajiwa kuanza Septemba 11.

Staa huyo alijiunga na Esperance Januari 2021 lakini alishindwa kutamba kama benchi la ufundi lilivyomtarajia, lakini Simba SC wanaamini mfumo wa Watunisia hao ulimfelisha.

Mshambuliaji huyo atajiunga na Simba SC huku kukiibuka sintofahamu ndani ya usajili wa Simba baada ya Meddie Kagere, Perfect Chikwende kuwa kwenye msafara. licha ya tetesi kusema kuwa wawili hao wapo kwenye orodha ya kuachwa.

Kambi ya Morocco kumnufaisha Matola kimasomo
Naibu Waziri aainisha manufaa ya anwani za makazi na postikodi