Julai 24, 2020, imekuwa siku yenye maumivu na majonzi kwa Watanzania, baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kulitangazia Taifa kuwa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa amefariki dunia.
Akiwa mwenye majonzi, Rais Magufuli alilieleza Taifa kuwa Rais Mstaafu, Mzee Mkapa amefariki katika hospitali jijini Dar es Salaam, alipokuwa anapatiwa matibabu. Lakini sentensi inayoweza kukuumiza zaidi ni uhalisia kuwa, “Mzee Mkapa hatunaye tena”. Rais ametangaza maombolezo ya kitaifa kwa siku saba, na bendera kupepea nusu mlingoti.
Nyota iliyong’ara, mwanga uliokorezwa na Mwenyezi Mungu kusaidia kulimulika Taifa la Tanzania akiliongoza tangu 1995 hadi 2005, na hata kumuona na kumuibua Rais wa sasa John Pombe Magufuli akiwa hana uongozi wowote ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imeanguka.
Ni Mzee Mkapa, nyota iliyokuwa pembeni tu, ikayagusa maono ya Muasisi wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, akaikumbuka kazi yake na kumuunga mkono kwa nguvu zote awe Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hakika Watanzania tumepoteza!
Pamoja na ung’aavu wa nyota hii iliyoacha historia kubwa kwenye Taifa letu. Mzee Mkapa amepitia mengi tangu alipozaliwa. Amevumilia mengi na mazito, akitembea kwa miguu umbali wa Kilometa 60 akiwa na mzigo kichwani akiifuata elimu. Hii ni kutokana na hali ya ufukara ya familia yake. Lakini bidii, ucha Mungu, kujifunza na kuwaheshimu watu vilimuinua.
Kutokana na mapenzi yake kwa Watanzania, Mzee Mkapa aliandika kitabu chenye kurasa 334, akielezea maisha yake kwa undani. Kitabu hicho kilichopewa jina la ‘My Life, My Purpose’, kwa tafsiri ya Kiswahili ‘Maisha Yangu, Kusudio Langu’, alikizindua Novemba 12, 2019, akiungwa mkono na Rais John Pombe Magufuli, marais wastaafu wenzake, Ali Hassan Mwinyi na Jakaya Mrisho Kikwete. Hii ilikuwa kumbukizi ya siku yake ya kuzaliwa, akitimiza umri wa miaka 81.
Katika uzinduzi wa kitabu hicho, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Prof. Rwekaza Mukandala, aliwasilisha uchambuzi na muhtasari wa kitabu hicho, kwa niaba ya Mzee Mkapa.
Na hivi ndivyo alivyoeleza:
Baba yake, Mzee Wiliam Matwani, alikuwa mpishi msaidizi katika misheni ya Ndanda, ambaye alifundishwa na wamisionari hadi kuwa katekista na baadaye kufundisha shule za ‘Bush’.
Mama hakuwa na muda wa kujifunza kusoma na kuandika kwani alikuwa msingi wa familia. Akihakikisha analima, kulisha familia na kuelea watoto. Alikuwa mkali lakini msikivu na mpenda haki,” Profesa Mkandala alisimulia.
Ingawa wazazi hawakwenda shule, alisema walipenda watoto wasome. Kipato kidogo cha uhakika kila mwezi kilifanya familia ionekane tofauti na kusababisha wivu na chuki.
Wivu na chuki vilisababisha tukio baya analolikumbuka kwa uchungu. Mwaka 1947 palitokea ukame mkali, watu wakamleta mganga wa kijijini ambaye alidai mama na bibi yake (Mkapa) waliloga kuzuia mvua. Hivyo, walipigwa na kuteswa sana hadi waliponasuliwa na Padri Mzungu. Bibi wa mama alifariki.
Kuitafuta elimu
Mkapa na mwenzie mmoja walichaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari kutoka kwenye darasa la watoto 25 hadi 30. Alieleza kuwa kwa wakati huo, kuchaguliwa ilikuwa bahati nasibu.
Shule ya Sekondari ya Ndanda ilikuwa umbali wa kilomita 60, walitembea kwa miguu bila viatu siku mbili wakiwa wamebeba vitu vyao vilivyofungwa kwa mkeka. Baadaye alipata sanduku la chuma. Baada ya kufika shuleni, alisema walimu walikuwa wamisionari walikazia sala na kazi na wanafunzi walipika chakula chao wenyewe.
Kwa kuwa Mkapa alikuwa mdogo sana, alipewa kazi ya kuosha vyombo. Kawaida alivibeba kichwani mpaka mahali pa kuoshea na kuvirudisha. Mkapa anasema kubeba vyombo hivyo ndiyo sababu ana upara hadi leo.
Alisema mwaka 1952 akiwa na umri wa miaka 15 alikwenda seminari darasa la nane, lakini baada ya muda mfupi aliona upadri si wito wake na alirudi Ndanda kuendelea na shule.
Mwaka 1957 alichaguliwa kwenda St. Fransis College (Pugu), ikiwa ni Shule Kuu ya Katoliki Tanzania.
Safari ya Siasa
Akiwa Pugu, Mkapa alipata mwamko wa siasa na aliunga mkono harakati za kudai uhuru na kuandika barua kwa Mhariri wa gazeti la The Tanganyika Standard ambalo sasa ni Daily News. Barua ilichapishwa lakini alitumia jina bandia.
Mkapa alishinda mitihani ya kujiunga na Chuo Kikuu Makerere akiwa kati ya wanafunzi watatu bora katika darasa la wanafunzi 51. Alikumbana na mambo mapya ikiwamo kucheza dansi ya kisasa. Hapo ilikuwa kazi na muziki. Na Mkapa aliendelea na harakati za kisiasa
Profesa Mkandala alieleza kuwa Mkapa alijiunga na Bodi ya Uhariri ya Gazeti la Transition, alikuwa mwanachama hai wa kikundi cha TANU, alishiriki siasa za chuoni, aligombea urais na kwamba ingawa hakushinda, wanafunzi wa kike walimpa kura nyingi kutokana na kujieleza kwake. Kutokana na sifa hizo, aliteuliwa makamu wa rais wa serikali ya wanafunzi na baadaye kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi. Alihitimu shahada ya lugha Aprili 1962.
Maisha na Kazi
Mkapa anamwelezea Hayati Mwalimu Julius Nyerere alivyounganisha nchi katika kupigania ukombozi wa Bara la Afrika, na anamtaja Mwalimu kama shujaa wake baada ya wazazi wake waliompigania akiwa mtoto.
Alisema alipenda kuajiriwa Wizara ya Mambo ya Nje. Alipewa sharti kuwa kama anataka nafasi hiyo, ingempasa kwanza kusomea masuala ya kidiplomasia. Aliajiriwa kama Bwana Mshauri Mkufunzi wa wilaya na alifanya kazi hiyo kwa miezi minne na baadaye alikwenda Colombia, Marekani kwa mwaka mmoja kusomea diplomasia. Baadaye aliajiriwa wizarani, kazi yake kuu ikiwa ni kuchukua muhtasari wa mazungumzo ya Rais na Waziri.
Alitumia muda wa ziada kusoma habari Radio Tanzania Dar es Salaam. Katika kipindi hicho, alimchumbia mkewe Anna.
Kuteuliwa Uhariri
Alisimulia kuwa, siku moja aliitwa Msasani kwa Mwalimu Nyerere na alimwambia amemteua kuwa Mhariri Mtendaji wa gazeti la The Nationalist. Kutokana na uteuzi huo, alikwenda Uingereza kujifunza mambo ya magazeti kwenye magazeti ya The Mirror. Alirejea na kufanya kazi chini ya Mwalimu akiwa Mhariri Mkuu.
Akiwa Mhariri Mkuu wa The Nationalist, Mkapa aliruhusiwa kuhudhuria mikutano mikuu ya kamati kuu ya Tanu, ambayo ilitawaliwa na malumbano ya hoja na uchambuzi yakinifu na alihusika kutayarisha sera mbalimbali za chama. Katika kipindi hicho, alisema alifundishwa ujamaa na alivutiwa na msimamo wa usawa na umuhimu wa kujitegemea. Alijiunga kwa hiari Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kuhitimu. Alieleza kuwa siku ya kuhitimu, Mwalimu Nyerere alikuwa mgeni rasmi na Mkapa alichaguliwa kusoma risala, na Mwalimu Nyerere alicheka sana alipoona amepungua sana.
Mwaka 1972, Mkapa aliteuliwa kuwa Mhariri Mtendaji wa Daily News na baadaye Katibu wa Rais na kuwa mwanzo wa maisha ya kisiasa na mwaka huo huo alimwagiza aanzishe Shirika la Habari Shihata, na yeye alikuwa Mtendaji Mkuu.
Mwaka 1976 aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Nigeria na mwaka mmoja baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na kuwa msaidizi wa Rais, akiwa pia mbunge wa kuteuliwa. Mwaka 1982 akawa Balozi wa Canada baadaye Marekani na baadaye Waziri wa Habari na Utamaduni na akarudi kuwa Waziri wa Nchi za Nje kuanzia mwaka 1984.
Mwaka 1995, Mkapa alichaguliwa kupeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi, akigombea Urais katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi nchini. Alishinda kwa kishindo akipata 61.82% dhidi ya Augustino Mrema (NCCR- Mageuzi) – 27.77%, Ibrahim Lipumba (CUF) – 6.43% na John Cheyo (UDP) – 3.97%.
Mwalimu Julius Nyerere, kwa imani yake kwa Mkapa, alizunguka nchi akimpigia kampeni, alimuombea kura kwa Watanzania akiwataka kumchagua kwani ni mtu safi, mwaminifu na mzaledo. Alikuwa Rais wa Tanzania kwa kipindi cha miaka 10, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alivyomuibua Magufuli:
Mzee Mkapa amewahi kusimulia jinsi alivyomuibua Rais John Pombe Magufuli, akiwa mbunge wa kawaida, asiye na cheo ndani ya CCM, lakini utendaji wake, upendo na ari ya kuchapa kazi vilimfanya ang’are.
“Katika utawala wangu nilivutiwa na Magufuli (Dkt. John Pombe Magufuli), kutokana na utayari wake, nguvu zake, ari yake, upendo wake, na moyo wake wa kujitoa na kutumikia, ndiyo maana mwaka 1995 nikamteua kuwa Naibu Waziri [wa Ujenzi], na baadaye kuwa waziri kamili (kuanzia mwaka 2000),” alisema Mzee Mkapa, Julai 10, 2017 alipozungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya hati za nyumba 50 zilizojengwa na Taasisi ya Benjamin Mkapa kwa Ufadhili wa Mfuko wa Dunia (Global Fund), wilayani Chato mkoani Geita.
Kutokana na jinsi alivyokuwa akichapa kazi na kuliongoza Taifa la Tanzania, amewahi kutunukiwa Shahada tisa (9) za heshima, na vyuo vinavyoheshimika duniani. Tangu mwaka 1998 hadi 2009, vyuo vilivyomtunukia shahada za heshima (Honorary degrees) ni pamoja na Chuo Kikuu cha Soka (Japan), Chuo cha Morehouse (Marekani), Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Chuo Kikuu cha Taifa (Lesotho), Chuo Kikuu cha Kenyatta (Kenya), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Tanzania), Chuo Kikuu cha Newcastle (Uingereza), Chuo Cha Cape Coast (Ghana), Chuo Kikuu cha Makerere (Uganda).
Mungu ametoa, Mungu ametwaa, jina la Mungu lihimidiwe.