Aliyekua Kaimu Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Thierry Hitimana amefunguka sababu za kushindwa kumtumia beki kutoka nchini Ivory Coast Serge Paschal Wawa, tangu alipokabidhiwa mikoba, baada ya kuondoka kwa Kocha Didier Gomes.
Kocha Hitimana amekiiongoza kikosi cha Simba SC katika mchezo mitatu ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Polisi Tanzania, Coastal Union na Namungo FC, huku chaguo lake katika safu ya ulinzi likiwa Henock Enonga, Kennedy Juma, Joash Onyango, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na Shomari Kapombe.
Hitimana amesema alilazimika kutomtumia Wawa, kutokana na hali halisi iliyokua ndani ya Kikosi cha Simba baada ya kupoteza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana.
Amesema beki huyo ambaye alihusika kufanya makosa na kupelekea mabao mawili ya Jwaneng Galaxy, alikosa amani na furaha baada ya kupoteza mchezo huo, hali ambayo ilimsababshia kuhemkwa kutokana na kushambuliwa kwenye mitandao ya jamii, hivyo yeye ni kama baba aliamua kumuweka mbali ili kumrejesha katika hali yake ya kawaida.
“Kelele zile zilimuathiri Wawa, kocha ni kama baba, niliamua kumuweka mbali na kelele hizo na uzuri amenielewa, ila bado ligi ni ndefu, Wawa atarejea uwanjani na atacheza mechi nyingi zilizo mbele yetu.” amesema Hitimana ambaye sasa anarejea katika nafasi yake ya Kocha Msaidizi kufuatia kuwasili kwa Kocha Pablo Frank Martin.
Kocha Pablo amewasili leo Jumatano (Novemba 10) asubuhi, na anatarajiwa kuanza kazi mara moja ili kukiweka sawa kikosi chake kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting utakaopigwa Novemba 19, Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.