Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar Hitimana Thiery amesema atakitumia kipindi hiki cha mapumziko ya Michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, ili kukiboresha kikosi chake.
Mtibwa Sugar imekua na matokeo mabovu kwa siku za karibuni, hali ambayo inaendelea kutoa mshangao kwa wadau wengi wa soka nchini, hasa baada ya kocha Hitimana kukabidhiwa kikosi hicho chenye maskani yake makuu Manungu, Turiani mkoani Morogoro.
Mtibwa haina matokeo mazuri kwani katika mechi zao 22 mpaka sasa imekusanya alama 24 tu ikiwa ni wastani wa kila mechi wanavuna alama moja na kutokana na kukusanya alama 24 na kukaa nafasi ya 15 na kuingia kwenye eneo la hatari ya kushuka daraja.
Kocha Hitimana amesema katika kuhakikisha wanafikia malengo yao walitoa mapumziko ya siku chache na tangu jana Jumatatu (Machi 16) timu ilirudi kambini kuendelea na mazoezi.
“Lazima tutumie muda huu kwa ufanisi, wachezaji wamerejea kambini kuendelea na program, lengo kubwa kujiweka fiti kwa ajili ya hizi mechi zilizobaki ili timu isalie Ligi Kuu msimu ujao,” amesema Thiery.
Kocha huyo Mnyarwanda ameongeza anafahamu mtihani alionao, kwani vita ya kukwepa kushuka daraja ni kali sana hivyo lazima kuwapo mpango mkakati wa kukwepa zahama hiyo.
Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea tena mwezi April, baada ya kupisha michezo ya kimataifa ya kufuzu fainali za mataifa ya Afrika, ambapo Tanzania itacheza dhidi ya Equatorial Guinea na Libya mwezi huu.