Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Kenya, Kithure Kindiki amesema Serikali imezifunga Shule za kutwa za msingi na upili katika maeneo ya Nairobi, Mombasa na Kisumu kutokana hofu ya usalama wa Wanafunzi inayotokana na tangazo la maandamano yaliyopangwa kufanywa na Muungano wa vyama vya upinzani.
Kindiki ameyasema hayo huku akiongeza kwamba Wizara ya Elimu itatangaza tarehe ya kurejelewa kwa masomo baada ya kutathiminiwa tena kwa hali ya usalama huku Azimio la umoja wakisema wataendelea na maandamano dhidi ya Serikali ya Rais, William Ruto kuanzia Julai, 19-21, 2023.
‘’Ni hatua ya tahadhari kuhakikisha usalama wa watoto wa shule, imeamuliwa kuwa shule zote za kutwa za msingi na upili ndani ya maeneo ya Nairobi na Mombasa (Jumatano, 19 Julai 2023) zitasalia kufungwa,’’ alisema Waziri Kindiki.
Akizungumza katika mkutano na vyombo vya Habari, Naibu wa Muungano huo ambaye pia alikua Mbunge wa Gichugu, Martha Karua alisema kwamba harakati za Muungano huo kuishinikiza Serikali kufutilia mbali mUswada wa fedha hazitasita, licha ya uwepo wa vitisho.