Mabingwa wa Soka nchini Nigeria Rivers United wameanza kuingiwa na ubaridi kabla ya mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Young Africans, huku nyota tishio ambao wamekuwa wakizungumzwa ni washambuliaji, Fiston Mayele na Stephane Aziz KI.
Young Africans imeondoka jijini Dar es salaam mapema leo Alfajiri kwenda nchini Nigeria kwa ajili ya mchezo huo utakaopigwa Jumapili (April 23) kwenye Uwanja wa Godswill Akpabio.
Akizungumza kutoka Nigeria, nyota wa Rivers na kinara wa mabao kwenye timu hiyo, Paul Acquah alisema wamejipanga kupambana vilivyo licha ya ubora wa nyota hao.
“Tuko tayari kupambana na timu nzima ila Mayele, Aziz Ki ni wachezaji wazuri, ambao sisi kama wachezaji ni lazima tujipange vizuri kukabiliana nao, tunahitaji kumaliza mechi hapa kwetu kabla ya mchezo wa marudia- no,” alisema Acquah mwenye mabao manne ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Naye Kocha Mkuu wa Rivers United Stanley Eguma amesema Young Africans waliyokutana nayo mwaka juzi ni tofauti na hii ya sasa, hivyo wanategemea mchezo mgumu ila malengo ni kuutumia vizuri uwanja wao wa nyumbani.
Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa Young Afrucans, Nesreddine Nabi, amekionya kikosi chake juu ya matumizi ya VAR, ambayo mabingwa hao wa Tanzania Bara watayatumia kwa mara ya kwanza.
Nabi amewataka wachezaji wake kuwa makini zaidi hata wanapokuwa na hasira na kudhani mwamuzi yupo mbali nao.