Kocha Mkuu wa Simba SC, Mbrazili Roberto Oliviera ‘Robertinho’ na wa Young Africans Muargentina Miguel Gamondi wote wataingia uwanjani wakicheza kwa kujilinda zaidi kwa kila mmoja akitaja ubovu wa uwanja ndio sababu.
Hiyo ni katika kuelekea mchezo wa Fainali ya Ngao ya Jamii itakayochezwa kesho Jumapili (Agosti 13) saa moja kamili kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Young Africans ndio ilikuwa ya kwanza kutangulia Fainali baada ya kuwafunga Azam FC mabao 2-0 kabla ya Simba SC juzi kuwaondoa Singida Fountain Gate kwa mikwaju ya penati baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu.
Akizungumza jijini Tanga Kocha Robertinho amesema kuwa, kikubwa kilichosababisha wao washindwe kupata ushindi katika mchezo huo dhidi ya Singida Fountain Gate ni uwanja kutokuwa rafiki kwao.
Robertinho amesema kuwa, anaamini hilo litatokea tena katika mchezo wa Fainali dhidi ya Young Africans, na hilo halitawatokea wao pekee, pia wapinzani watakutana na kero hiyo ya ubovu wa uwanja.
“Nimefurahishwa na jinsi timu yangu kufuzu kucheza Fainali ya Ngao ya Jamii, nawapongeza wachezaji wangu kwa kupambana na kupata ushindi.
“Kwani katika mchezo huo, tulicheza kwa tahadhari kubwa ya kujilinda na kufanya mashambulizi ya kushitukiza kutokana na uwanja wenyewe kutokuwa rafiki kwetu Simba SC na wapinzani wetu Singida,” amesema Robertinho.
Gamondi naye mara baada ya mchezo dhidi ya Azam alisema kuwa: “Niwapongeze wachezaji wangu kwa kucheza soka safi, licha ya uwanja kutokuwa rafiki na kusababisha muda mwingi kutumia mashambulizi ya kushitukiza.
“Licha ya ubovu huo wa uwanja, tutajitahidi kupambana kadiri ya uwezo wetu kwa kushirikiana na wachezaji wangu kufanikisha malengo ya kubeba Kombe la kwanza msimu huu,” amesema Gamondi.